• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:10 PM
Wananchi kufaidika baada ya ERC kupunguza bei ya umeme

Wananchi kufaidika baada ya ERC kupunguza bei ya umeme

Na BERNARDINE MUTANU

TUME ya Kudhibiti Kawi (ERC) imepunguza gharama ya matumizi ya umeme kwa watumiaji wa kawaida.

Wakati wa mkutano na wanahabari jana, ERC ilitangaza kupunguza malipo kwa watumiaji wa kilowati kati ya 10 na 100 kwa mwezi hadi Sh10 kutoka Sh12 kwa kila kilowati moja.

Ilipotangaza bei mpya Julai, Wakenya walio na mapato ya wastani walioathiriwa na bei mpya ya umeme baada ya kuondolewa katika orodha ya wananchi waliofaa kulipa Sh10 kwa kila kilowati.

Malipo hayo mapya yataanza kutekelezwa leo baada ya ERC kuondoa ushuru wa mafuta, ushuru wa ubadilishaji wa fedha za kigeni na ushuru wa utumiaji wa umeme.

“Tume imebadilisha malipo kwa watumiaji wa umeme manyumbani kwa lengo la kuwafaa zaidi wakazi wa mitaa ya mabanda, wakazi wa mijini na masoko na maeneo ya mashambani,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa ERC, Pavel Oimeke.

Alisema lengo kuu ni kuwapunguzia wananchi gharama ghali ya maisha.

Hatua hiyo itawafaidi wananchi wapatao 5.7 milioni kote nchini.

Wakenya wengi wamekuwa wakilalamikia ongezeko la gharama ya maisha kutokana na ushuru ambao umekuwa ukiongezwa kwa bidhaa za kimsingi mara kwa mara.

Ongezeko hilo la ushuru hasa limesababishwa na mzigo wa madeni ambayo Kenya inalipa mataifa ya kigeni kwa mikopo iliyochukua.

You can share this post!

Sheria mpya ya SACCO yaibua tumbojoto Kiambu

Mpango wa ANC, Ford-K kuungana wasambaratika

adminleo