Habari Mseto

Gavana ahimiza vyombo vya habari vikabili ugaidi

November 1st, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na MANASE OTSIALO

Gavana wa Mandera Ali Roba ameomba vyombo vya habari kujiunga na kampeni dhidi ya ugaidi, baada ya kampeni hiyo kuzinduliwa hivi majuzi katika kaunti hiyo.

Akiongea wakati wa mkutano na maafisa wakuu kutoka Shirika la Habari la Nation wakiongozwa na Afisa Mkuu Msimamizi Bw Steven Gitagama, Bw Roba alisema vyombo vya habari vina wajibu wa kupinga simulizi kuhusu ugaidi.

“Hivi majuzi tulizindua kampeni ya kumaliza misimamo mikali Mandera na vyombo vya habari vina wajibu mkubwa katika vita dhidi ya al-Shabaab,” alisema.

Kulingana na Bw Roba, wakati vyombo vya habari vinaposema ukweli kuhusu dhana ya kigaidi inayosambazwa na makundi ya kigaidi, wananchi wanaweza kuelewa ukweli.

“Vyombo vya habari lazima vipate ukweli kuhusu ugaidi ili tuishi bila woga kwa lengo la kukuza kaunti yetu, na taifa kwa jumla,” alisema.

Kulingana na ripoti, magaidi wengi hutumia Mandera kuingia nchini kupanga na kutekeleza mashambulizi ya kigaidi nchini.

“Mandera imehusishwa katika mashambulizi yote ya kigaidi nchini. Lakini wakati vyombo vya habari vinapozungumzia athari za ugaidi, tutashinda sisi wote,” alisema.

Vyombo vya habari vinafaa kubadilisha mtazamo kuhusu ugaidi Mandera, mtazamo ambao umefanya Mandera kuonekana kama kaunti adui nchini.

“Tuna changamoto lakini tunahitaji kuelewa kuwa changamoto hii sio kwetu pekee na tunafaa kueleza katika habari zetu,” alisema Bw Roba.

Bw Gitagama aliahidi kuongoza Shirika la Habari la Nation kufanya kampeni ya kupigia debe Mandera iliyo salama kwa kujiunga na kampeni hiyo.

“Tuko hapa kuhakikisha kuwa tumeungana mkono katika kampeni ya kuhakikisha kuwa Mandera ni salama na kushirikiana katika shughuli nyingine ambazo zitaibua mabadiliko mazuri,” alisema.

Bw Gitagama aliteuliwa hivi majuzi kama mkurugenzi mkuu wa Nation kuchukua mahali pa Joe Muganda, ambaye alikuwa katika wadhifa huo tangu Julai 2015.

Bw Gitagama alijiunga na NMG Septemba 2007 kama Mkurugenzi Mkuu wa Fedha kutoka kampuni ya kutengeneza pombe ya Kenya Breweries Ltd, ambako alikuwa na wadhifa kama huo.

Ni mhasibu aliyeidhinishwa na ana digrii ya uzamili katika usimamizi wa kibiashara na digrii ya biashara (uhasibu) kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.