Wakazi wa Lamu kunufaika na huduma za Kenya Power
Na BERNARDINE MUTANU
Kampuni ya Kenya Power imeanzisha ushirika kati yake na Serikali ya Kaunti ya Lamu kwa lengo la kuimarisha maisha ya wakazi wa kaunti hiyo.
Kampuni hiyo itasakini taa kubwa za mtaani katika Kaunti ya Lamu.
Pia, kampuni hiyo itashirikiana na kaunti hiyo katika ujenzi, uendeshaji na udumishaji wa muundo msingi wa stima, biashara ya umeme, uundaji wa sera katika sekta ya kawi, ajira na uhifadhi wa umeme, ilisema kampuni hiyo katika taarifa.
Kaunti ya Lamu imejiunga na kaunti zingine 16 ambazo zimetia sahihi mikataba na Kenya Power ili kuwekewa taa mitaani kwa lengo la kuimarisha usalama na uchumi kwa saa 24.
Mradi wa taa mitaani ulianza 2014 na umefaidi miji kama vile Nairobi, Mombasa, Kisumu, Nyeri, Eldoret, Nakuru na Machakos miongoni mwa miji mingine mikuu.
Kufikia sasa masoko na vituo 500 vya kibiashara vimefaishwa na mradi huo.
Baadhi ya masoko yamefadhiliwa na serikali ya kitaifa na mengine yamefadhiliwa na serikali za kaunti.
Serikali ya kitaifa imetoa KShs.13.5 bilioni katika utekelezaji wa mradi huo na kufikia sasa mipango ya thamani ya KSh 6.8 bilioni inaendelea.