• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 2:07 PM
LSK kukabiliana na mawakili bandia

LSK kukabiliana na mawakili bandia

Na ERIC MATARA

CHAMA cha Wanasheria nchini(LSK) kimeanza juhudi za kuanzisha kitengo cha ukaguzi ili kukabiliana na mawakili bandia ambao wamekuwa wakiwatapeli wateja.

Afisa Mkuu Mtendaji wa chama hicho, Bi Mercy Wambua, jana alifichua kuwa wamewasilisha mapendekezo bungeni ambayo yakipitishwa yataruhusu kubuniwa kwa idara ya kukabiliana na mawakili matapeli.

Bi Wambua alisema kwamba LSK imeanza msako kote nchini wa kuwakamata watu wanaohudumu kama mawakili kinyume cha sheria.

“Matapeli wanaojifanya mawakili walio na leseni wamekuwa mwiba kwa LSK. Hata hivyo, tumejitolea kuanzisha sheria kadhaa ili kuwazuia. Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuanzisha kitengo cha ukaguzi ili kuhakikisha taaluma hii haiingiliwi na matapeli,” alisema Bi Wambua. Akikiri kwamba tatizo la mawakili bandia lipo na ni changamoto kwa LSK, Bi Wambua alisema kwamba chama kinatafuta mbinu za kuwakomesha nchini.

“LSK haitakubali matapeli waharibu jina zuri la taaluma yetu. Kwa sasa tunashirikiana na wizara ya ardhi, sekta ya kibinafsi, polisi na mahakama kuhakikisha wamekamatwa,” alisema.

“Matapeli wanaochafua jina la taaluma hii watakamatwa na kukabiliwa kisheria,” alisema.

Alisema tayari LSK huwa kinachapisha habari kuhusu kila wakili katika tovuti yake.

Afisa huyo alishauri wateja kuhakikisha ikiwa mtu ni wakili halali kabla ya kutafuta huduma zake.

Iliibuka kuwa chama hicho tayari kinashirikiana na mahakimu, majaji na maafisa wa usalama kuwakamata matapeli wanaojifanya mawakili.

“Kupitia matawi yetu kote nchini, tumesambaza orodha ya mawakili walio na leseni. Itakuwa rahisi kuwakamata na kuwashtaki walaghai kuliko ilivyokuwa awali. Tuko na maafisa wa usalama wa kuwasaka matapeli katika mahakama na nje ya mahakama pia.”

alieleza.

Chama hicho pia kimeanza mpango wa kuhamasisha Wakenya kuhusu huduma za sheria ili waweze kuepuka matapeli. Kwa wakati huu, kuna zaidi ya mawakili 16,000 waliosajiliwa na LSK.

Watu wanaojifanya mawakili wamekuwa wakikamatwa na kushtakiwa kwa kujifanya wanasheria kwa nia ya kulaghai umma. Mnamo 2013 LSK kilitoka orodha ya mawakili na kampuni za mawakili ambazo kilisema walikuwa wakihudumu kinyume cha sheria maeneo ya Kisii, Rongo, Migori, Kilgoris, Nyamira, Thika, Kajiado na Kitengela

You can share this post!

Aambia korti mkewe huombea bangi kabla ya kuivuta

Hofu Kisauni ikidaiwa polisi wamegeuka majambazi

adminleo