• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
ODM yapuuzilia mbali ziara ya Ruto

ODM yapuuzilia mbali ziara ya Ruto

JUSTUS OCHIENG na RUSHDIE OUDIA

VIONGOZI wa Chama cha ODM Jumanne walipuuzilia mbali ziara ya Naibu Rais William Ruto katika maeneo ya Kusini mwa Nyanza Jumatatu, wakaeleza sababu zao za kutoandamana naye.

Mwenyekiti wa ODM ambaye pia ni Mbunge wa Suba Kusini iliyo Kaunti ya Homa Bay, Bw John Mbadi, alisema afisi ya Naibu Rais haikujali hata kualika viongozi wa maeneo aliyozuru na badala yake walioalikwa walikuwa ni wabunge wa zamani ambao hawawakilishi wakazi wa maeneo hayo.

“Inafaa ifahamike wazi kwamba Ruto hakutualika. Ujumbe pekee niliopokea kuhusu ziara yake ulitoka kwa kamishna wa kaunti Ijumaa na ziara ilipangiwa kuwa Jumatatu. Kwa hivyo sijui aliamua wakati gani kufanya hii ziara,” akasema Bw Mbadi jana.

Aliongeza: “Ruto ana afisi ambayo ina wafanyakazi wa kutosha na inafadhiliwa kwa ushuru wetu. Jambo la busara zaidi ambalo angefanya ni kutualika kwa mkutano Nairobi ili tujadiliane naye kuhusu masuala yanayokumba watu wetu.”

Alimkosoa pia kwa kuzindua miradi ya zamani ambayo imekuwa ikiendelezwa.

Kwa upande wake, Seneta wa Homa Bay, Bw Moses Kajwang’ ambaye alimlaki seneta mwenzake wa Baringo, Bw Gideon Moi katika kaunti hiyo wiki iliyopita, alisema hangehudhuria mkutano wa naibu rais kwa kuwa hayuko nchini kwa sasa.

Mbunge wa Homa Bay, Bw Peter Kaluma, alisema anamkaribisha rais na viongozi wengine wote kuzuru kaunti yake, lakini hakufahamishwa wala kualikwa kuhudhuria hafla za Bw Ruto.

“Inasikitisha kwamba Naibu Rais alipiga picha tu katika miradi ya zamani akatangaza Sh20 milioni pekee zitatumiwa kwa Hospitali ya Tom Mboya Level 4 iliyo Rusinga, ilhali yeye hutenga mabilioni ya fedha za taifa kwa miradi ya maeneo mengine,” akasema.

Alisema Bw Ruto hakuzungumzia kuangamiza gugumaji katika Ziwa Victoria, kusitisha uagizaji wa samaki kutoka Uchina na kuboresha uzalishaji wa samaki wa kufugwa, wala kutolewa kwa Sh780 milioni ambazo ziliwekwa kwa ujenzi wa uwanja mdogo wa ndege wa Kabunde ulio Homa Bay katika mwaka wa 2013/2014.

You can share this post!

Walimu 15 kuzuiliwa kuhusiana na wizi wa KCSE

Askofu na pasta kizimbani kwa madai ya ulaghai

adminleo