Makala

TAHARIRI: Gharama ya kilimo nchini ipunguzwe

November 7th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

KUNA suala ambalo linakanganya kuhusu usimamizi wa kilimo hapa nchini.

Inakuwa vipi wafugaji wa kuku wa mayai nchini Uganda wanaweza kuuza mayai yao hapa Kenya kwa bei ya chini kuliko ya wafugaji wa hapa Kenya?

Bei hii inakuwa ya chini licha ya kuwa na gharama za kusafirisha mayai hayo hadi maeneo mbalimbali ya Kenya. Hali ni vivyo hivyo kwa maziwa, mahindi na mazao mengine yanayotoka Uganda.

Hali hiyo ni sawa kwa wakulima wa vitunguu, machungwa na nanasi kutoka Tanzania ama wauzaji samaki kutoka China, mahindi kutoka Mexico na sukari kutoka Brazil licha ya umbali wa nchi hizo kutoka Kenya.

Hii ni aibu kubwa kwa Kenya kama taifa na hasa kwa serikali kwa kushindwa kustawisha sekta ya kilimo, ambayo ndiyo tegemeo kubwa zaidi kwa idadi kubwa ya Wakenya sehemu za mashambani, na yenye uwezo wa kupunguza umaskini nchini kwa kiwango kikubwa.

Kiini kikuu cha wakulima wa Kenya kushindwa kushindana na wenzao kutoka nchi za kigeni ni gharama za juu za kuzalisha mazao, kutokana na bei za juu za mbegu, mbolea, vyakula vya mifugo na dawa za wadudu.

Hali hii imekuwepo kwa muda mrefu na serikali haijaonyesha nia yoyote ya kusaidia kupunguza bei hizi, na badala yake imekuwa ikitenda kinyume kwa kuongeza kodi kwa bidhaa hizi.

Kumekuwepo na mipango ya mbolea ama mbegu nafuu lakini hili sio suluhisho ikizingatiwa mfumo wa kugawa bidhaa hizi umejaa ufisadi na ubaguzi, na matokeo yake ni kuwa mkulima anayelengwa hanufaiki.

Suluhisho la kwanza kwa matatizo ya wakulima ni kuchukua hatua za kimakusudi kupunguza gharama za uzalishaji mazao kwa kushusha ushuru na kupunguza kodi kwa watengezaji wa bidhaa hizi.

Hatua hizi zitahakikisha kuwa Wakenya wanazalisha chakula kwa gharama nafuu na hivyo kuwasaidia kushindana na wakulima wengine duniani.

Hili pia litahakikisha idadi kubwa zaidi ya wananchi watakuwa na uwezo wa kununua chakula kwa bei nafuu, hali itakayoimarisha hali ya afya nchini.