Kaunti yachunguza askari waliovamia mwanahabari aliyerekodi video wakimeza hongo
Na VALENTINE OBARA
SERIKALI ya Kaunti ya Nairobi imeanzisha uchunguzi kuhusu tukio ambapo mwanahabari alidai kupigwa na askari wa kaunti akiwa kazini.
Bw Kimani Mbugua, ambaye ni mwandishi habari wa Runinga ya Citizen, alipigwa na walinzi wa kaunti hiyo Jumanne katikati mwa jiji alipokuwa akinasa video kuhusu ulaji rushwa kutoka kwa wahudumu wa bodaboda.
Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Mkurugenzi wa Huduma za Habari katika kaunti, Bw Elkana Jacob, alisema maafisa husika watashtakiwa iwapo uchunguzi utabainisha walikiuka sheria.
“Serikali ya kaunti hii haistahimili ufisadi na suala hilo litachunguzwa kwa kina. Maafisa husika watatendewa haki lakini endapo watapatikana na hatia, watashtakiwa,” akasema.
Bw Mbugua ambaye amelazwa hospitalini baada ya kupata majeraha mabaya shingoni alikuwa amesimulia jinsi maafisa hao walimshambulia.
Kulingana naye, aliona maafisa wakiitisha hongo kutoka kwa mhudumu wa boda boda ambaye alikuwa ameingia katikati mwa jiji kinyume cha sheria za kaunti zinazoharamisha marufuku boda boda kuingia mjini ndipo akaanza kunasa tukio hilo kwenye simu yake ya mkononi.
Licha ya kujitambulisha kuwa ni mwanahabari, alinukuliwa kusema watu hao ambao hawakuwa wamevalia sare za kazi walimwonyesha vitambulisho vyao vya kazi kisha kumpeleka kwenye afisi zao na kuanza kumpiga na kumlazimisha kufuta video alizonasa kabla kumwachilia.
Gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko, amekuwa akisisitiza kwamba uendeshaji boda boda katikati mwa jiji ni marufuku ingawa agizo hilo limepuuzwa kwani askari wa jiji huwaruhusu wahudumu kuingia jijini badala ya kuendeshea shughuli zao pembezoni mwa mji wanakostahili kuwa kisheria.
Wakati mwingi, wahudumu wa boda boda hukiuka sheria za trafiki kwani wao huziendesha katika upande wa barabara usiofaa na hawafuati mwelekeo wa taa za trafiki, hali inayoweka hatarini maisha ya watumiaji wengine wa barabara, hasa wapita njia.
Wahudumu hao pia huegesha pikipiki zao katika sehemu za barabara zisizostahili na hivyo basi kutatiza shughuli jijini.
Wakati mmoja, Bw Sonko alisikitishwa na jinsi baadhi ya maafisa wa kaunti hukusanya ada kutoka kwa wahudumu wa boda boda na pia kutoka kwa wachuuzi ambao hawastahili kuwa mjini ili kuwaruhusu kuendesha biashara hizo kwa njia haramu.
Ingawa alikuwa ameagiza mkuu wa idara ya usalama wa kaunti achukulie hatua maafisa wanaotenda ufisadi huu, tukio la juzi ambapo mwanahabari huyo alidhulumiwa linaonyesha kuwa bado hatua mwafaka hazijachukuliwa.
Hata hivyo, kwenye taarifa yake, Bw Jacob alisema kuna pia watu ambao hujifanya kuwa askari wa usalama wa kaunti ilhali ni walaghai wanaotapeli wafanyabiashara na wananchi.
“Tunafahamu kuna watu kadhaa ambao hujidai kuwa maafisa wa kaunti, na hii ni changamoto inayoshughulikiwa. Madai hayo yatachukuliwa kwa uzito unaostahili,” akasema.