• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:30 PM
Wabunge Rift Valley wamtaka Ruto aache kuwa kigeugeu

Wabunge Rift Valley wamtaka Ruto aache kuwa kigeugeu

Na ONYANGO K’ONYANGO

WANDANI wa Naibu Rais William Ruto katika ngome yake ya kisiasa ya Rift Valley, wanataka atangaze msimamo wake halisi kuhusu mwafaka wa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga.

Wabunge hao wanataka pia Bw Ruto aeleze wazi msimamo wake kuhusu mapendekezo ya kurekebisha katiba.

Wakizungumza Jumapili, walisema hali ya Bw Ruto kutokuwa na msimamo kuhusu masuala hayo inaweza kuathiri umaarufu wake anapojiandaa kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika 2022.

“Naibu Rais anafaa sasa awe na msimamo thabiti kuhusu ‘handsheki’ na mabadiliko ya katiba kwa sababu haya ni masuala ambayo Wakenya wanafuatilia kwa makini.

“Akiendelea kuwa kigeugeu kuhusu masuala haya mawili, ataweka azimio lake la kisiasa hatarini,” akasema Mbunge wa Cherang’any, Bw Joshua Kutuny, kwenye majohiano na Taifa Leo.

Walizungumza siku moja tu baada ya Bw Ruto kusema yuko tayari kushirikiana na Bw Odinga, ambaye ni hasimu wake wa kisiasa, kwenye uchaguzi wa 2022.

Wiki chache zilizopita, alibadili msimamo wake kuhusu marekebisho ya katiba ambayo alikuwa awali anapinga vikali kwa kudai kuwa ni njama ya Bw Odinga na wandani wake kutafuta njia ya kuingia serikalini kupitia ‘mlango wa nyuma’.

Mbunge wa Nandi Hills, Bw Alfred Keter, alimwambia naibu rais kwamba msimamo wake kuhusu mambo hayo mawili utaamua kama atashinda urais au la.

“Naibu Rais na wafuasi wake wanafaa wawe na msimamo. Mabadiliko ya katiba yatahakikisha kuna usimamizi bora wa serikali na kuzuia ufisadi,” akasema Bw Keter.

Hata hivyo, wandani wake wengine walimtetea na kusema msimamo wa Bw Ruto unajulikana wazi na unafaa kuheshimiwa na kila mmoja.

Seneta wa Nandi, Bw Samson Cherargei, na Mbunge wa Soy, Bw Caleb Kositany, walisema naibu rais tayari ameonyesha nia njema kuhusu ‘handsheki’ na juhudi za kupambana na ufisadi.

Wawili hao walisema safari ya Bw Ruto kuelekea Ikulu haiwezi kuzuiliwa kwa sababu Chama cha Jubilee tayari kiliamua yeye ndiye atapeperusha bendera ya chama hicho ifikapo 2022.

You can share this post!

SHERIA ZA MICHUKI: Hakuna mjadala kuhusu sheria kwa matatu

Wandani wa Ruto wakashifu mahasimu kutoa ushahidi mpya...

adminleo