Akasha waugua wakiwa gerezani jijini New York
Na KEVIN J KELLEY
NDUGU Baktash Akasha na Ibrahim Akasha, ambao wanazuiliwa nchini Amerika kwa ulanguzi wa mihadarati, wanaugua.
Habari kutoka mahakama ya Amerika walikoshtakiwa zinasema kuwa Baktash anaugua maradhi ya kisukari na shinikizo la damu huku Ibrahim akizongwa na mawazo na amekuwa akipewa ushauri nasaha katika rumande ya New York ambapo amekuwa akizuiliwa kwa miezi 21 sasa.
“Ibrahim Akasha anaugua maradhi ya mzongo wa mawazo,” wakili wa Baktash alimwambia Jaji Kathleen Parker aliyekuwa akisikiza kesi dhidi yao.
Wakili wa upande wa utetezi George Goltzer, aliitaka mahakama kuagiza Ibrahim ahamishiwe katika rumande ambayo ndugu yake Baktash anazuiliwa jijini New York City ili waweze watiane motisha.
Jaji Parker alikubali kushauri Idara ya Magereza ihamishe Ibrahim hadi katika rumande ambapo Baktash anazuiliwa.
Ndugu hao walikiri katika korti ya New York kuwa walanguzi wa dawa za kulevya na sasa wanasubiri hukumu.
Nakala za korti zinaonyesha kuwa Baktash na Ibrahim walikiri kuwapa hongo wanasiasa, polisi na majaji ili kukwepa mkono wa sheria nchini Kenya.
Ndugu hao pia walikiri kumhonga mwendesha mashtaka mmoja nchini Kenya katika jaribio lao la kutaka wasisafirishwe hadi nchini Amerika ambapo wanakabiliwa na mashtaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya.
Wawili hawa hata hivyo hawakutaja majina ya maafisa wa polisi, majaji au waendesha mashtaka waliopewa hongo.
Ndugu hao huenda wakahukumiwa kifungo cha kati ya miaka 10 hadi maisha gerezani.
Naibu mwendesha mashtaka wa Amerika, Amanda Houle aliambia korti kuwa wawili hawa walitumia mamilioni ya fedha walizopata kutokana na ulanguzi wa dawa za kulevya kuwahonga wanasiasa, waendesha mashtaka na majaji nchini Kenya.
Houle alisema kuwa shehena ya kilogramu 500 ya heroini ilikuwa safarini wakati ndugu hao walipotiwa mbaroni miaka minne iliyopita nchini Kenya kabla ya kusairishwa hadi Amerika mwaka jana.
Jaji Parker alisema kuwa Jaji Victor Marrero atakayeamua kesi hiyo alionya kuwa ndugu hawa huenda wakapewa adhabu kali zaidi kuliko inavyotarajiwa.
Baktash Akasha, 41, na Ibrahim Akasha, 29, waliambia Jaji Parker kwamba hawakuahidiwa msamaha na upande wa mashtaka kabla ya kukiri mashtaka hayo.
Kulingana na maafikiano kati ya waendesha mashtaka na ndugu hawa wawili, huenda wakatozwa faini ya Sh5 milioni na milioni Sh1 bilioni.
Akasha pia walikubali kukabidhi kwa serikali fedha walizojipatia kupitia kwa ulanguzi wa mihadarati.