Kimataifa

Museveni akaangwa kusema kazi ya upishi ni ya wanawake

November 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

RAIS wa Uganda Yoweri Museveni amekabiliwa vikali baada ya kutumia matamshi kuwa sehemu ya jikoni katika nyumba ni ya wanawake, akisema kuwa tangu alipooa hajawahi kuingia jikoni kwa kuwa kazi ya kupika ni ya wanawake.

Akizungumza kueleza haja ya watumishi wa umma kufanya kazi ambazo wamepewa haswa bila kufanya majukumu yaw engine, Rais Museveni alitumia mfano wa upishi nyumbani nasehemu ya jikoni, akisema kuwa mwanaume hafai kupika.

“Kiongozi wa boma hafai kuingia jikoni. Sasa nimeishi miaka 45 na mama Janet na sijawahi kukanyaga jikoni. Hivyo ndivyo inafaa kuwa,” akasema kupitia ujumbe.

Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya kimataifa ya Oxfam Winnie Byanyima alikashifu matamshi ya Rais huyo wa miaka 74 kupitia mtandaowa Twitter, akisema namna alivyoghadhabishwa.

“Upishi si kazi ya mwanamke. Ni kazi ya kimaisha. Watu wote- wanaume kwa wanawake wanafaa kupika,” Bi Byanyima akaandika “Wakati wa kupika, kuosha na kufanya kazi nyingine za nyumbani zinaachiwa wanawake, wananyimwa nafasi sawa ya kufanya kazi za mapato ama kuwa na usemi wa kisiasa.”

Beatrice Alaso wa chama cha Opposition Forum for Democratic Change alieleza AFP kuwa Rais huyo alidhihirishia dunia namna hawathamini wanawake.

“Museveni amedhihirisha kile amekuwa akiamini; kuwa wanawake hawawezi kutoshana na wanaume wenzao.”

Lakini shirika moja la habari za mitandao nchini humo lilimtetea Museveni kuwa alipiga mwangwi tu Imani na itikadi za Waganda ambao wanaamini kuwa mwanaume hafai kupika.