Kimataifa

TEKNOLOJIA: Mtangazaji wa kwanza roboti duniani mmakinifu na asiyechoka

November 13th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

MASHIRIKA na PETER MBURU

WUZHEN, China

SHIRIKA moja la habari China limeanza kutumia huduma za mtangazaji wa habari ambaye si binadamu, ila roboti, ambaye atakuwa akisoma habari saa 24 kwa siku.

Shirika la Xinhua lilianza kutumia roboti hilo ambalo ni zao la teknolojia, likiitwa mtangazaji wa Artificial Intelligence katika kongamano la mtandao, Jiji la Wuzhen.

Roboti hilo lilisoma habari kwa Kiingereza siku hiyo likianza kama wasomaji wa kawaida wanavyosoma “Hamjambo, mnatazama habari za kimombo. Mimi ni msomaji wa habari AI nikiwa Beijing.”

Roboti hilo ambalo liliundwa na Xinhua na kampuni ya intaneti ya China lina umbpo la kuakisi sura, sauti na hisia za uso za binadamu.

“Msomaji AI anajisomesha mwenyewe kutokana na video za matangazo ya moja kwa moja na anaweza kusoma jumbe fupi kikawaida na kitaalamu kama wasomaji wa habari maarufu,” shirika la Xinhua likasema.

Shirika hilo lilisema roboti hilo litatumiwa katika akaunti zake za mitandao ya kijamii na kuwa hali hiyo itapunguza gharama na kupandisha viwango vya ubora.

Hata hivyo, bado si wazi ikiwa mashirika ya habari yanayomilikiwa na serikali nchi hiyo yatatumia huduma za roboti kutekeleza kazi zake.

Roboti hilo liliumbwa kufanana na kuiga kila kitu cha mtangazaji halisi wa Xinhua kwa jina Zhang Zhao.

“Nitafanya kazi bila kuchoka ili kuwafahamisha kwani jumbe zitaandikwa ndani yangu bila matatizo yoyote,” likasema roboti hilo, kupitia video ya kujitambulisha.

Katika kongamano hilo, roboti jingine ambalo limemwiga mtangazaji wa shirika hilo la Xinhua lilizinduliwa.

Lakini watumizi wa mtandao ambapo habari hizo zilichapishwa hawakuridhishwa kikamilifu kuwa mtangazaji huyo roboti ana utaalamu wa kutosha.

Wengine walitafsiri hali hiyo kuwa watangazaji sasa wataanza kupoteza kazi zao ikiwa maroboti yameanza kuzifanya.

Hii si mara ya kwanza kwa Xinhua kujaribu matumizi ya teknolojia ya AI, kwani 2015 roboti lilitumiwa kutoa matangazo ya hali ya anga wakati wa asubuhi