Kimataifa

Mbwa apiga kambi barabarani siku 80 baada ya mmiliki wake kufa

November 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

MASHIRIKA na PETER MBURU

MBWA mmoja nchini China amevuta hisia za watu wengi, baada ya kukaa sehemu ya barabara ambayo mmiliki wake alifariki kwa siku 80 akimsubiri arudi.

Kanda za video zimemwonyesha mbwa huyo akihangaika katika eneo la Hohhot, Mongolia katika sehemu ya barabara, kanda ambayo imetazamwa mara 1.4 milioni katika mtandao wa Sina Weibo.

Tovuti hiyo ilisema mbwa huyo amekuwa katika sehemu hiyo ya barabara kila siku tangu mmiliki wake alipofariki dunia mnamo Agosti 21.

Dereva mmoja wa teksi alisema watu wamejaribu kumsaidia mbwa huyo lakini kila mara anatoroka.

“Madereva humpa chakula mbwa huyo lakini kila tunapotoka kwenye gari anatoroka. Uhusiano kati ya mbwa huyo na mmiliki wake ulikuwa thabiti sana. Baada yake kuuawa, mbwa huyo mdogo amekuwa akisimama hapo tu.”

Tangu kanda ya video ya mbwa huyo kurekodiwa na kuwekwa katika mtandao wa Sina Weibo ambao hutumiwa kama Facebook, watumiaji wameshikwa na huruma na kuzungumza kuhusu uaminifu wa mbwa huyo kwa mmiliki wake.

Mbeleni, mbwa huyo amedaiwa kuwa alikuwa na uhusiano wa karibu sana na mmiliki wake, kiwango kuwa alikuwa akimsubiri kila wakati walipotoka kazini ili aende nyumbani pamoja.

Kisa cha uaminifu wa mbwa huyo kwa binadamu kimeibuwa kumbukumbu za wanyama hao wengine ambao wamewahi kuonyesha mapenzi na uaminifu wao kwa wamiliki kwa kuwa na uhusiano wa karibu sana.