Habari Mseto

Baridi yailazimisha KQ kupunguza safari za Amerika

November 14th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na BERNARDINE MUTANU

Shirika la Uchukuzi wa Ndege (KQ) limepunguza idadi ya safari za moja kwa moja kwenda Marekani siku chache baada ya kuzindua safari hizo.

Kulingana na shirika hilo, idadi ya watu wanaofanya ziara za Marekani imepungua kutokana na kuwa ni msimu wa baridi.

KQ imepunguza ziara hizo kati ya Oktoba 28, 2018 hadi Machi 30, 2019, “Tumefutilia mbali ziara zote ambazo hazina faida, hili sio jambo jipya,” alisema afisa wa KQ.

Shirika hilo tayari limefutilia mbali ziara 10 ambazo zilikuwa zimepangiwa kati ya Novemba 5 na Desemba 5.

Inatarajiwa kuwa ziara zaidi zitaathiriwa kabla ya msimu wa baridi kuisha. Hata hivyo KQ haikutangaza siku kamili za safari zilizofutiliwa mbali.

KQ imejitetea kwa kusema hiyo ni hatua inayokubaliwa kote kwa lengo la kuejiepushia hasara wakati biashara inapoenda chini.

Ilisema wote walioathiriwa na hatua hiyo walifahamishwa majuma matatu kabla ya ziara ya moja kwa moja hadi Marekani kuzinduliwa.

Hata hivyo, jedwali la ziara zake za moja kwa moja hadi Marekani halijabadilishwa, lilisema shirika hilo.