Kampuni 5 zaungana kuwafaa wakulima wa viazi
Na FAUSTINE NGILA
KAMPUNI tano zimeungana kwa nia ya kuwasaidia wakulima wa viazi kukuza kilimo chao, kama mbinu ya kuhakikisha kuwa kuna chakula cha kutosha nchini.
Kupitia mradi wa Better Life Project, kampuni za Bayer East Africa, TingA, Yara, Siraji SACCO na Farmer Centre Limited zinapanga kuwapa wakulima mbegu bora, kuhimiza utumiaji wa mashine katika kilimo na kutumia mbolea za bei nafuu ili kuhakikisha kuwa viazi havivamiwi na wadudu.
“Lengo letu sio tu kuuza mbolea bali pia kuwauzia wakulima mbolea inayohitajika kulingana na mchanga wa eneo Fulani,” akasema Vitalis Wafula, meneja katika kampuni ya Yara.
Kampuni ya TingA nayo ilisisitiza kuwa matumizi ya mashine kwenye kilimo yatawasaidia wakulima wa viazi nchini kuvuna mara tano ya mazao ambayo wanavuna sasa.
“Matumizi ya mashine za kuvuna viazi hupunguza vikubwa hasara zinazokuja wakati wa mavuno kwa kuwa viazi vyote vinatolewa mchangani na kuna viini vichache vya uharibifu wa chakula hicho,” akasema meneja katika kampuni hiyo, Mhandisi Titus Musyoka.
Baadhi ya wakulima tayari wamesifia hatua hiyo kuwa imeboresha mavuno katika mashamba yao, baada ya kutumia mbegu zinazofaa.
“Wamekuwa wakituelekeza katika kilimo chote cha viazi na kuhakikisha kuwa tunafanya kila kinachohitajika hadi wakati wa kuuza mazao. Wametembelea hata mashamba yetu kwa ukaguzi na kutoa idhini kabla ya upanzi wa mbegu Fulani. Mbeleni nilikuwa nikivuna kati ya magunia 15 na 30, lakini sasa ninavuna kati ya 70 na 100,” akasema Amos Ngugi, mkulima kutoka Nanyuki.