Kibaki asheherekea miaka 87 kimya kimya nyumbani kwake
Na GRACE GITAU
RAIS Mstaafu Mwai Kibaki jana alisheherekea miaka 87 tangu kuzaliwa kwake katika makazi yake ya kifahari mtaani Muthaiga, Nairobi.
Hata hivyo msemaji wake Ngare Gituku alikataa kufichua au kutoa maelezo zaidi kuhusu sherehe hizo akizitaja kama za kibinafsi.
Ingawa hivyo, Wakenya hawakusita kujitosa kwenye mitando ya kijamii kumtakia Rais Mstaafu heri njema, wengi wakitaja miradi ya maendeleo iliyotimizwa wakati wa utawala wake.
Wakati huo huo, afisi ya Bw Kibaki imepuuzilia mbali ripoti kwamba Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga alipata idhini kutoka kwa Bw Kibaki ili kubadilisha jina la Hospitali ya Othaya Level Six hadi hospitali ya rufaa na mafunzo ya Mwai Kibaki.
Kulingana na habari zilizozambaa kwenye mitandao ya kijamii, Bw Kahiga na Mbunge wa Othaya Gichuki Mugambi waliafikiana kuhusu hilo baada ya mkutano na Bw Kibaki nyumbani kwake Mweiga, kaunti ya Nyeri majuma mawili yaliyopita.
Bw Gituku hata hivyo amekanusha kutojua lolote kuhusu mkutano unaodaiwa kufanyika huku afisi ya gavana ikisisitiza kwamba mkutano huo ulifanyika.