• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
TAHARIRI: Masoko zaidi ya mazao yasakwe

TAHARIRI: Masoko zaidi ya mazao yasakwe

NA MHARIRI

Taarifa ya Wizara ya Biashara, Viwanda na Ushirika kwamba, wafanyabiashara wa Kenya wataanza kuuza maparachichi moja kwa moja nchini China kuanzia Januari ni ya kutia moyo na kila juhudi zinapasa kufanywa kufanikisha mpango huo.

Kwa miaka mingi, kumekosekana uwiano wa kibiashara huku China ikiuzia Kenya bidhaa za thamani ya mabilioni kila mwaka. Isitoshe, mashirika ya China yamekuwa yakinufaika na zabuni kubwa hasa katika sekta ya ujenzi na miundomsingi kwa jumla.

Kwa upande mwingine, wakulima na wafanyabiashara wa Kenya wamewekewa msururu wa vizingiti ambavyo vimetatiza juhudi zozote za wakulima hao kuuza bidhaa zao nchini China.

Kwa vyovyote vile, hizi bila shaka ni habari nzuri, ikizingatiwa kuwa Kenya iliipiku Afrika Kusini mwaka jana na kuuza avocado za thamani ya Sh.7.8bilioni na hivyo kuifanya muuzaji mkubwa zaidi wa avocado Uchina.

China ni nchi kubwa, yenye idadi kubwa ya watu na uchumi thabiti. Kuna njia nyingi Kenya inaweza kuvuna pakubwa kutokana na ushirikiano huo mpya wa kibiashara.

Kwa mfano, mbali na avocado, kaunti za Kitui na Makueni huzalisha mbaazi kwa wingi. Ama kweli, msimu uliopita, wakulima wa mbaazi walivuna zao hilo kwa wingi lakini wakakosa soko baada ya mpango wa awali wa kuiuzia India kutibuka.

Vile vile, kaunti za Kisii na Nyamira hukuza ndizi kwa wingi. Itakuwa vyema iwapo mikakati itafanywa kuhakikisha masoko ya bidhaa za Kenya yanapanuliwa tusiwe tunategemea masomo maalumu pekee, hasa wakati huu ambapo Shirika la Kibiashara Duniani (WTO) liliondoa Kenya kutoka mataifa yanayoendelea.

Hatua hiyo ilimaanisha bidhaa kutoka Kenya vinakuwa ghali ikingalishwa na vile vya mataifa jirani ambavyo vinatozwa ushuru wa chini.

Wito wetu ni kwa Rais Kenyatta kuendeleza kampeni binafsi ya kutafutia bidhaa za Kenya, hasa vya kilimo katika mataifa ya kigeni ili wakulima wetu wapate msukumo wa kuzalisha mazao hayo kwa wingi.

Mfano bora ni kufufua uzalishaji wa zao la pareto. Tunaamini kuna mataifa mengi yanaweza kununua zao hilo kwa wingi endapo serikali itaingilia kati kwa wakati ufaao.

Kwa mara nyingine, tunampongeza Waziri Peter Munya kwa juhudi hizo ambazo bila shaka zitakuwa na manufaa makubwa kwa raia wa Kenya na uchumi wa nchi kwa jumla.

You can share this post!

KINAYA: Raia wa kawaida ni kama wakimbizi nchini mwao,...

MOHAMMED: Muafaka wa Uhuru na Raila hakika ni laana ya aina...

adminleo