Habari Mseto

Matibabu ya figo yaanza Lamu

November 16th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

NA KALUMEKAZUNGU

KAUNTI ya Lamu kwa mara ya kwanza katika historia imeanzisha matibabu ya figo kufuatia kuzinduliwa rasmi kwa vifaa maalum vya kutekelezea tiba hiyo na Waziri wa Afya nchini, Sicily Kariuki Ijumaa.

Kaunti hiyo pia imefungua chumba cha kisasa cha upasuaji na pia kile cha kupiga picha mifupa ya mwili kwa kutumia tarakilishi (CT-Scan) huku mashini zote zinazotumiwa kwenye idara hizo zikifadhiliwa na serikali ya kitaifa.

Akizungumza kwenye uwanja wa hospitali kuu ya kaunti-King Fahad mjini Lamu Ijumaa, Bi Kariuki alisema jumla ya Sh 1.1 bilioni zimetumika katika ununuzi wa vifaa hivyo.

Bi Kariuki alisema kaunti ya Lamu ni mojawapo ya maeneo ambayo yamekuwa yakishuhudia changamoto za kimiundomsingi hasa kuhusiana na masuala ya afya.

Alisema serikali kuu itaendelea kujitolea kwa hali na mali ili kuhakikisha wakazi wa eneo hilo wanapokea huduma bora za afya.

Alisema kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Lamu, ofisi yake itatuma wataalamu wa matibabu hivi karibuni ili kukagua jinsi mashini hizo zinavyofanyiwa kazi na pia kuangazia jinsi huduma za afya zinatolewa kwa wananchi kwa jumla kwenye hospitali na zahanati mbalimbali za eneo hilo.

Waziri wa Afya nchini, Sicily Kariuki alipozindua matibabu ya Figo Novemba 11, 2018 Lamu. Picha/ Kalume Kazungu

“Nafurahia kuwa hapa Lamu leo kuzindua kitengo cha matibabu ya figo. Huu ni mwamko mpya kwa kaunti ya Lamu ambayo imekuwa ikishuhudia wagonjwa wengi wakihama eneo hili kutafuta tiba ya figo kwenye maeneo ya Malindi, Mombasa na hata Nairobi.

Kufunguliwa kwa kitengo cha matibabu ya figo eneo hili kutapunguza matatizo ambayo wagonjwa wa figo hukumbana nayo wakati wakitafuta tiba. Kwa sasa watatibiwa figo papa hapa Lamu,” akasema Bi Kariuki.

Waziri huyo wa Afya pia aliahidi kutuma majokofu maalum ya kuhifadhia chanjo na pikipiki eneo hilo ili kutumiwa na Maafisa wa Matibabu ya Kijamii katika kusambazia watoto chanjo.

Alisema idadi ya watoto wanaopokezwa chanjo kaunti ya Lamu bado iko chini.

“Ili kuboresha kiwango cha chanjo kwa watoto wasiozidi umri wa miaka mitano eneo hili, ofisi yangu itatuma majokofu zaidi hya kiuhifadhia chanjo hiyo na pia pikipiki zitakazowasaidia maafisa wa huduma za matibabu ya kijamii kusafiri wakifikisha chanjo maeneo ya mashinani. Hatua hiyo ni katika harakati za kuboresha zaidi idadi ya watoto wanaopokezwa chanjo kutoka asilimia 77 hadi kiwango cha kitaifa ambacho ni angalau asilimi 82. Furaha yetu ni kuona watoto wote wanapata chanjo eneo hili,” akasema Bi Kariuki.

Naye Gavana wa Lamu, Fahim Twaha, aliipongeza serikali ya kitaifa kwa juhudi zake katika kuboresha huduma za afya kwa wakazi nchini.

Bw Twaha alisema kaunti pia iko mbioni katika kuimarisha huduma zinazotolewa hospitalini na pia kupunguzia wananchi wa eneo hilo gharama.

“Tunafurahia kwamba kwa mara ya kwanza Lamu itaanza kutoa matibabu ya figo. Tunaipongeza serikali chini ya Rais Uhuru Kenyatta kwa juhudi zake katika kuboresha huduma za afya eneo hili. Kaunti pia imejikakamua na tayari tunaendelea na usajili wa family 20,000 zitakazofadhiliwa na kaunti katika bima ya afya ya hospitali (NHIF) mwaka huu,” akasema Bw Twaha.