• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Waluhya kamwe hawawezi kuungana, asema Khalwale

Waluhya kamwe hawawezi kuungana, asema Khalwale

Na BENSON AMADALA

JUHUDI za kuunganisha jamii ya Waluhya ili kuunda vuguvugu la kisiasa litakalotoa mgombea urais mwaka 2022 zimegonga kisiki tena kufuatia hatua ya aliyekuwa seneta wa Kakamega Boni Khalwale kumuunga mkono Naibu wa Rais William Ruto.

Bw Khalwale ambaye sasa amegeuka ‘kijana wa mkono’ wa Naibu Rais sasa anautaja muungano wa Waluhya kuwa ndoto, akisema hakuna uwezekano wa juhudi za kuunganisha vyama vya ANC na Ford Kenya kufaulu.

Seneta huyo ambaye mbeleni alikuwa katika mstari wa mbele kupigania jamii hiyo kushikamana ili kuwa na usemi kisiasa sasa ameacha kampeni hizo, na badala yake amechukua msimamo ambao viongozi wa magharibi wanakerwa nao, wa kuwataka wamuunge mkono Bw Ruto.

“Nimejaribu sana kuunganisha ANC na Ford Kenya ili jamii ya Waluya ipange safari ya kisiasa ya 2022 mapema lakini viongozi wa vyama wamekuwa wakichelewesha shughuli hiyo sana,” akasema Dkt Khalwale.

Alisema japo pamoja na Katibu Mkuu wa ANC Barrack Muluka waliunda ripoti kuhusu suala hilo na kuwasilisha kwa viongozi wa vyama Musalia Mudavadi na Moses Wetangula, viongozi hao wanajikokota tu.

Aliongeza kuwa kutokana na kufishwa moyo na hali hiyo ndipo aliamua kumuunga mkono Bw Ruto. Lakini majuzi Bw Khalwale amenukuliwa akimtaka Bw Mudavadi kumuunga mkono naibu wa Rais, wito ambao kinara huyo wa ANC ameupinga vikali.

Lakini kwa upande mwingine, viongozi wengine wa eneo hilo wamemlaumu Bw Khalwale kwa changamoto zinazoshuhudiwa katika juhudi za kuunganisha jamii hiyo, wakimtaja kuwa kisiki kinachozuia jamii kuungana na kusema kuwa anatumia ajenda hiyo kumpigia debe Bw Ruto.

“Kile tunaambiwa kuwa kuunganishwa kwa ANC na Ford Kenya hakuna. Kimekufa. Khalwale amekuwa akitumia maneno hayo ili kuendeleza ajenda yake ya kumuunga mkono William Ruto,” akasema seneta wa Kakamega Cleophas Malala.

Bw Muluka naye amemkosoa Bw Khalwale kwa kusema kuwa juhudi za kuunganisha jamii hiyo zimekufa, akisema hakujakuwa na kikao chochote baina ya viongozi wa jamii hiyo na uamuzi wa aina hiyo kuafikiwa.

Hata hivyo, bado kimya kinasalia kutoka vinara wakuu Mudavadi na Wetangula, ikiwa kwanza wako tayari kuvunja vyama vyao na kuungana, jambo ambalo linawacha kila kitu angani.

You can share this post!

Hatimaye Mutua akubali kushirikiana na Ngilu na Prof Kibwana

Kalonzo naye afika kwa Mzee Moi kusaka baraka

adminleo