• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Ruto achunguzwe kuhusu sakata ya mahindi – Wabunge wa Rift Valley

Ruto achunguzwe kuhusu sakata ya mahindi – Wabunge wa Rift Valley

Na STANLEY KIMUGE

WABUNGE watatu wa Jubilee kutoka Bonde la Ufa sasa wanataka Naibu wa Rais William Ruto achunguzwe kuhusiana na sakata za mahindi na mbolea, ambazo zilisababisha mabilioni ya pesa za umma kupotea.

Wabunge Alfred Keter wa Nandi Hills, Joshua Kuttuny wa Cherangany na Silas Tiren wa Moiben jana walisema kuwa Bw Ruto anafaa kujitokeza wazi kusafisha jina lake kuhusiana na sakata hizo ambazo zilikumba sekta ya kilimo na nusra ziizoroteshe katika kipindi cha miaka michache ambayo imepita.

“Hizi shida zote zinatokana na Naibu wa Rais na ofisi yake. Tunataka ofisi yake ichunguzwe na wale walioingiza mbolea duni nchini na mahindi waeleze Wakenya kwa nini waliingiza bidhaa hizo.

“Huwezi kuwa ukiwaambia wakulima wa humu nchini wakuze parachichi ilhali hutaki kutuambia kilichofanyika na mahindi kwa kuwa wewe ni sehemu ya tatizo. Na ikiwa unadhani kwamba tunakosea jitokeze utukosoe,” Bw Keter akasema.

Wabunge hao walikuwa wakizungumza wakati wa mkutano wa wakulima katika kituo cha Tacs, ili kutafuta mwelekeo kuhusiana na changamoto ambazo wakulima wamekuwa wakikumbana nazo.

Bw Kuttuny alidai kuwa naibu wa Rais pamoja na ofisi yake wamehusishwa katika uchunguzi unaoendelezwa kwa sasa kuhusiana na sakata hizo.

Bw Kuttuny aliendelea kudai kuwa Bw Ruto amekuwa akiwatafuta maafisa wa Bodi ya Kitaifa ya Uhifadhi wa Nafaka (NCPB) ili kuficha ukweli.

“Tunataka naibu wa Rais achunguzwe kwa kuwa tumesikia kwamba amekuwa akiwapigia simu maafisa wa NCPB akiwaamrisha namna ya kuwalipa waliowasilisha mahindi. Aidha, tumewasilisha miswada bungeni lakini bado ameingilia kati ili kuhakikisha kwamba haifanikiwi,” akasema mbunge huyo wa Cherangany.

Vilevile, Bw Keter alitaka aliyekuwa waziri wa Kilimo Willy Bett aamrishwe kuelezea Wakenya kile kimekuwa kikiendelea ndani ya wizara hiyo kwa miaka mitano iliyopita. Bw Bett awali mwaka huu aliteuliwa kuwa balozi wa Kenya nchini India.

Bw Tiren alisema kuwa viongozi wote akiwemo Bw Ruto wanafaa kukaguliwa hali ya maisha yao, ili kutatua tatizo kwenye sekta ya mahindi.

Wakati wa mkutano huo wa jana, viongozi hao walitoa makataa ya wiki mbili kwa serikali kununua mahindi ya wakulima kwa bei ya Sh3,600 kila gunia la kilo 90 msimu huu, la sivyo wawachochee wakulima kuandamana hadi Jijini Nairobi kukutana na Rais Uhuru Kenyatta.

Wiki iliyopita, idara ya uhifadhi wa vyakula maalum ilikuwa imetangaza kununua mahindi kwa Sh2,300 lakini wakulima hawakuridhika na bei hiyo.

Viongozi hao walisema kuwa watu wanaopiga domo kuwa wakulima wajihusishe na kilimo cha mimea mbalimbali mbadala ndio walihusika pakubwa na sakata ya mahindi.

Vilevile, waliwakosoa magavana wa eneo hilo kwa kukosa kuanzisha kiwanda cha usagaji wa mahindi ambacho kinaweza kusuluhisha shida ambazo wakulima wanapitia.

“Magavana wetu hawana uwazi na wakazi. Wamekuwa wapi miaka mitano iliyopita,” akasema Bw Kuttuny huku naye Bw Keter akirejelea kauli kuwa kuondolewa kwake na wenzake kutoka uwenyekiti wa kamati za bunge ulikuwa sehemu ya mpango mpana wa kupora pesa za wakulima.

You can share this post!

Mabapa mapya ya magari yaanza kutolewa

PWANI: Siasa za viuno zilivyotenganisha Jumwa na Mboko

adminleo