Habari Mseto

KURUNZI YA PWANI: Kampeni kuhusu mimba za mapema yazinduliwa

November 19th, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na FADHILI FREDRICK

NAIBU Gavana wa Kwale Bi Fatuma Achani ameanzisha kampeni itayojumuisha wanawake katika juhudi za kupambana na mimba za mapema kwa wasichana wa shule.

Bi Achani alisema kampeni hiyo itahusisha wanawake katika vitengo vyote vya vijiji 77 kupitia programu ya uhamasishaji.

Mpango huo unafuatia idadi kubwa ya wasichana wadogo iliyoripotiwa kupachikwa mimba kote nchini kama ilivyoonekana wakati wa mtihani wa KCPE na mtihani unaoendelea wa KCSE ambapo wasichana kadhaa walifanya mtihani wao hospitalini na hata wengine kukosa mtihani huo.

Kaunti ya Kwale pekee ilikuwa na wanafunzi wawili wa kike waliofanya mtihani wao wa KCPE hospitalini baada ya kujifungua.

Bi Achani alisema mimba za mapema kwa vijana zimekuwa tishio kubwa kwa elimu ya wasichana nchini, akisistiza umuhimu wa kukabiliana na changamoto hiyo.

“Tunalenga kujumuika pamoja katika Kampeni ambayo itahusisha kuwawezesha wazazi na wasichana kiuchumi,” akasema.

Kampeni hiyo imepigwa jeki na baadhi ya mashirika ya kijamii ambayo pia yana malengo kuhamasisha wasichana kuepukana na mimba za mapema.

Takwimu zilizotolewa na shirika la Moving the Goalpost (MTG) zinaonyesha asilimia 40 ya wasichana wadogo kaunti hiyo wako na ujauzito.

Mkurugenzi wa MTG, Bi Dorcus Amakobe, amesema ukosefu wa habari juu ya afya ya uzazi ndio moja wapo inayosababisha mimba na ndoa za mapema na hata vijana wengi hawajui mabadiliko yao ya kimwili.

Bi Amakobe anasema katika juhudi za kuelimisha vijana juu ya mimba za mapema, shirika hilo limesajili wasichana 800 chini ya mpango wa uwezeshaji kwa njia ya michezo na kwamba lengo lao ni kuwasajili wasichana wengi zaidi.

“Tunalenga kuandikisha wasichana wengi iwezekanavyo ili waweze kufaidika na mpango huu kwa kuwa unawapa fursa ya kujifunza kuhusu afya ya uzazi wao,” akasema.

Pia aliongeza kuwa wako na mpango wa kutoa huduma kwa wasichana kwenye vituo vya afya kwa ushauri juu ya Ukimwi na magonjwa ya zinaa.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Kwale Welfare and Education Association (KWEA) Bi Sabina Saiti amewahimiza wazazi kuwaongoza watoto wao vizuri kuwa na malengo katika maisha na kutoa msaada katika kufikia malengo yao.

Alieleza kuwa wazazi wanamchango mkubwa katika kuwalea watoto wao na hawapashwi kulaumu walimu kwa kushindwa kuwakuza watoto wao vyema.

“Idadi ya mimba za mapema inaweza kuwa kubwa zaidi kuliko kile tunachosikia. Ukweli ni kwamba watoto wanafanya mahusiano ya ngono wakati wakiwa nyumbani kama wazazi hawawafuatilii hasa wakati wa likizo, “akasema.

Alibainisha kuwa ikiwa wazazi hawana makini na watoto wao, kuna uwezekano wa matukio mengi ya ujauzito kuripotiwa Januari kwani watoto wengi huenda wakajihusisha na ngono wakati wa likizo ndefu ya Disemba.

Bi Saiti aliwahimiza wazazi kuhakikisha watoto wao wanafanya kazi wakati wa likizo na kuwaepusha kujihusisha na watu wenye malengo ya kuwaharibia maisha yao.

Pia aliwaonya wazazi kutokuwa chanzo cha watoto kuiga tabia mbaya Kutokana na matendo yao, Kwani familia nyingi hufanya watoto wao kuwa kitega uchumi.

“Kuna wazazi wanaohusika na wanaokosa maadili na hivyo basi kusababisha watoto wao kupotaka kimaadili,” akasema akiongeza kuwa watoto wengine hata wanalazimika kufanya ukahaba ili kuhudumia mahitaji yao ya familia.