• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 4:10 PM
2022: Mbinu mpya ya Raila kuzoa kura za Mlima Kenya

2022: Mbinu mpya ya Raila kuzoa kura za Mlima Kenya

Na JOSEPH WANGUI

ALIYEKUWA Waziri Mkuu, Raila Odinga, anaonekana kutumia mbinu mpya za kichinichini kushawishi eneo la Mlima Kenya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Mikutano yake ya mara kwa mara na viongozi kutoka eneo hilo, imeibua maswali kuhusu anacholenga katika ngome ya Rais Kenyatta ambayo kwa miaka mingi huwa inamchukulia kama mwiba kisiasa.

Tangu aliposalimiana na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi 9 na kuwa na muafaka, Bw Odinga amekutana na wanasiasa na makundi tofauti tofauti kutoka Mlima Kenya mara 13 kufikia sasa.

Mikutano hiyo imeibua maswali huku baadhi ya watu wakibashiri kwamba huenda Bw Odinga akagombea urais kwa mara ya tano ifikapo 2022. Kuna wasiwasi eneo hilo kwamba huenda kura za eneo hilo zitagawanyika kwenye uchaguzi mkuu ujao tofauti na ilivyokuwa kwenye chaguzi za 2007, 2013 na 2017.

Kabla ya kuingia katika muafaka na Rais Kenyatta, eneo hilo lililo na kura zaidi ya 6 milioni kutoka Kaunti zake 10 lilionekana kuegemea upande wa Naibu Rais William Ruto.

Hii ilitokana na matamshi ya Rais Kenyatta wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka jana kwamba eneo hilo litamuunga Bw Ruto baada ya kukamilisha vipindi vyake viwili 2022.

 

Kabando wa Kabando

Lakini aliyekuwa mbunge wa Mukurweini Kabando wa Kabando ambaye ni mmoja wa wabunge wa zamani waliokutana na Bw Odinga Juni 27 2018, alitetea mkutano huo akisema ulihusu juhudi za kuunganisha nchi.

“Ni wanasiasa wachache wanaopiga vita juhudi za Uhuru na Raila kuunganisha Wakenya. Kwa bahati nzuri, wananchi wengi pamoja na wawekezaji watajika wanafurahishwa na vita dhidi ya ufisadi na muafaka huo ambao umeleta amani nchini Kenya,” alisema Bw Kabando.

Aliongeza: “Mbinu ya kumtusi Raila iliyotumiwa na eneo la Mlima Kenya imetupiliwa mbali. Wale wanaotaka kutambuliwa sasa wanaendelea kumtusi yule ambaye tumeamua kumuunga mkono bila masharti na kuupigia debe muafaka. Ikiwa makosa yetu ni kuunga uamuzi wa UhuruRaila, basi makosa yetu hayo ndiyo ambayo nchi hii inahitaji,” alisisitiza.

Kulingana na Bw Kabando, kutokana na muafaka, nchi sasa imegawanyika katika makundi mawili: moja linalounga vita dhidi ya ufisadi ili ajenda Nne Kuu za Rais Uhuru ziweze kufaulu na pili ni kundi linalohujumu vita dhidi ya ufisadi ili ajenda hizo zikose kufaulu na kumfanya kuwa rais aliyeshindwa kutekeleza majukumu yake.

“Tumechagua kuwa na Uhuru hadi mwisho na kukubali muafaka wake na Raila ili nchi yetu iungane na kustawi,” aliongeza.

Viongozi kutoka eneo hilo waliokutana na Bw Odinga hivi punde ni Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru, kundi la viongozi kutoka Embu wakiongozwa na aliyekuwa mbunge Joe Nyagah na waliokuwa wabunge 12 kutoka Kaunti za Meru na Tharaka-Nithi wakiongozwa na aliyekuwa mbunge Kilemi Mwiria.

 

Uungwaji mkono

Baada ya kukutana na Bw Odinga, viongozi kutoka Tharaka Nithi na Embu, waliahidi kuunga mageuzi ya Katiba na kuunganisha nchi.

“Ingawa Raila alisema kwamba hatagombea urais 2022, kundi hili linakwambia kwamba unafaa kugombea na tutakuunga mkono,” walisema kwenye taarifa ya pamoja iliyosomwa na Kilemi Mwiria ambaye alikuwa mbunge wa Tigania Magharibi.

Wengine waliomtembelea Bw Odinga ni mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria, aliyekuwa kiongozi wa Mungiki Maina Njenga na aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo.

Naibu Rais William Ruto, ambaye analenga kumrithi Rais Kenyatta 2022, amekuwa akitembelea eneo la Mlima Kenya na kufanya harambee mara kwa mara. Tangu uchaguzi mkuu uliopita, Bw Ruto ametembelea eneo hili mara 38.

Mbinu za wanasiasa hao wawili zimezua mjadala kuhusu mwelekeo ambao eneo la Mlima Kenya litachukua baada ya Rais Kenyatta kukamilisha vipindi vyake vya kuhudumu.

“Kura za eneo la Mlima Kenya ndizo zitakazong’ang’aniwa sana 2022 na yeyote atakayogombea urais. Na kufikia sasa ni Naibu Rais aliyetangaza kwamba atagombea urais. Hakuna mtu mwingine mashuhuri ambaye ametangaza kugombea wadhifa huo,” alisema mbunge wa Nyeri mjini Ngunjiri Wambugu.

Bw Wambugu alisema kwamba kile ambacho Bw Ruto anafanya kwa wakati huu ni kujaribu kuziwahi kura za Mlima Kenya kabla ya mgombeaji mwingine wa urais kuzifikia.

 

Maendeleo

“Ikiwa atafaulu au la sijui kwa sababu watu wa Mlima Kenya huwa makini sana na fikira zao. Tumekuwa na mtu kutoka eneo hili akiwa Rais kwa miaka kumi iliyopita. Tumekuwa na maendeleo japo si vile tulitaka hasa katika kipindi chake cha kwanza, tunatarajia kwamba Uhuru atafanya mengi zaidi katika kipindi chake cha pili katika eneo hili,” alisema Bw Wambugu.

Kulingana Wambugu, kila mgombeaji wa urais 2022 atalazimika kuwaambia wapigakura wa eneo la Mlima Kenya atakayowatendea na si yale ambayo serikali ya Jubilee imetenda.

Lakini mbunge wa Imenti Kaskazini Rahim Dawood, ambaye ni mfuasi sugu wa Bw Ruto anasema kwamba naibu rais ndiye mgombeaji maarufu zaidi eneo hilo na wapigakura tayari wanamuunga mkono.

Bw Dawood alisema kwamba ziara za Bw Ruto eneo hilo huwa za maendeleo na wala si za kisiasa.

“Ruto huja hapa kufanya maendeleo na kuhakikisha kuwa wananchi hawamsahau. Ingawa maendeleo ni haki ya kila mtu, akija, huwa tunamkumbusha mahitaji yetu na ahadi walizowapa wapigakura kwenye kampeni za uchaguzi wa 2017,” alisema Bw Dawood.

Mbunge huyu aliongeza kuwa Bw Ruto huwa anatumia miradi ya maendeleo kuvumisha serikali ya Jubilee na kukagua miradi inayoendelea.

You can share this post!

Salah, Mane, Koulibaly, Benatia na Partey kuwania...

Mshahara wa Sanchez unavyozidi kuzua tumbo joto Trafford

adminleo