• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
JAMVI: Ni mlima kwa Ruto kumnasa Mudavadi

JAMVI: Ni mlima kwa Ruto kumnasa Mudavadi

Na LEONARD ONYANGO

BAADA ya kiongozi wa chama cha ODM Bw Raila Odinga na mwenzake wa Wiper Bw Kalonzo Musyoka kunaswa na Rais Uhuru Kenyatta, sasa Wakenya wameelekeza macho kwa kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi.

Ni dhahiri kuwa juhudi za Bw Mudavadi kuunganisha wapiakura wa Magharibi zimeambulia pakavu na sasa amejipata njiapanda kisiasa.

Atakumbukwa kwa kupendekeza wazo la muungano wa NASA, kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017, na kufaulu kuwashawishi Mabw Odinga, Kalonzo na Wetang’ula kuungana naye kwa na kupeperusha bendera ya muungano huo kwenye uchaguzi huo uliokumbwa na utata.

Baada ya Bw Odinga kutangaza kushirikiana na Rais Kenyatta mnamo Machi 9, 2018, Mabw Musyoka, Mudavadi na kiongozi wa Ford-Kenya Moses Wetang’ula walituma taarifa kwa vyombo vya habari wakisema kuwa wataendeleza ajenda ya upinzani ya kupigania masilahi ya Wakenya bila kiongozi huyo wa ODM.

Bw Kalonzo tayari ametangaza kushirikiana na Rais Kenyatta na hata kupewa jukumu la ubalozi wa amani nchini Sudan Kusini.

Chama cha Ford Kenya kinachoongozwa na Bw Wetang’ula na aliyekuwa seneta wa Kakamega Boni Khalwale ambaye ni naibu kiongozi wa chama, kinaonekana kuegemea mrengo wa naibu wa Rais William Ruto.

Tayari Dkt Khalwale ametangaza waziwazi kuunga mkono Bw Ruto katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

Sasa Bw Khalwale anataka Naibu wa Rais kuteua mmoja wa viongozi wa Magharibi, Bw Mudavadi au bw Wetang’ula kuwa mwanaiaji mwenza wake wa urais katika uchaguzi mkuu ujao.

Ukaribu wa viongozi wa viongozi wa Ford Kenya na Bw Ruto tayari umesambaratisha mpango wa kutaka kuunganisha chama hicho na kile cha Amani National Congress (ANC) chake Musalia Mudavadi.

Chama cha ANC tayari kimemtaka Bw Wetang’ula kujitenga na Bw Ruto ikiwa kabla ya kuunganisha vyama hivyo viwili.

Bw Mudavadi amesisitiza kuwa hatakubali wadhifa serikalini.

“Siko tayari kuchukuwa wadhifa wowote serikalini,” akasema Bw Mudavadi ambaye wiki iliyopita alikutana usiku na naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee David Murathe na kuzua minong’ono kwamba huenda akatunukiwa wadhifa na Rais Kenyatta.

Ripoti zinaonyesha kuwa Bw Murathe alikutana na Bw Mudavadi kwa takribani saa saba nyumbani kwake katika eneobunge la Gatanga, Kaunti ya Murang’a.

Kulingana na wadadisi wa masuala ya kisiasa, ukuruba uliopo baina ya familia Rais Mstaafu Daniel Moi na Bw Mudavadi haurusu makamu wa rais wa zamani kuunga mkono Bw Ruto.

“Sawa na Rais Kenyatta, Bw Mudavadi aliingizwa katika siasa na Mzee Moi. Hivyo ni vigumu kwa Bw Mudavadi kuunga mkono Bw Ruto na kuacha Seneta wa Baringo Gideon Moi ambaye ametangaza kuwania urais 2022,” anasema Wakili Felix Otieno.

“Ni rahisi kwa Bw Mudavadi kukubali kupewa wadhifa na Rais Kenyatta kuliko kuunga mkono Bw Ruto,” anaongezea.

Bw Moi amekuwa akizunguma maeneo ya Ukambani na hata Nyanza ili kujitafutia uungwaji mkono.

Wakili Ahmednasir Abdullahi anasema kuwa Wakenya watakuwa na imani na Bw Mudavadi iwapo atasimama kidete na kukataa kuunga mkono Bw Ruto na hata kupewa wadhifa na Rais Kenyatta.

“Wakenya tayari wamepoteza imani na Bw Odinga na bw Musyoka. Endapo Bw Mudavadi atasimama kidete hadi mwisho ataaminika na kukubalika zaidi miongoni mwa Wakenya ikilinganishwa na vigogo wenzake wa NASA,” anasema Bw Abdullahi.

You can share this post!

MOKAYA: Bado Guardiola ni mkali kuliko Mourinho

USAJILI KDF: Wanawake wafungiwa nje

adminleo