Habari Mseto

KCPE: Shule ilichomeka lakini hawakufa moyo

November 21st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na SAMMY KIMATU

KUCHOMEKA kwa shule yao siku mbili tu kabla ya mtihani, kusomea madarasa yaliyojengwa kwa mabati ndani ya mtaa wa mabanda wa Mukuru kwa Njenga na kutoka familia maskini kwenye mtaa huo ni changamoto nyingi kwa wanafunzi wa Siloam Education Centre.

Lakini matatizo hayo kamwe hayakuzima ndoto za watahiniwa wa shule hii baada ya 61 kati yao kupata alama 350 na zaidi kwenye mtihani wa mwaka huu wa KCPE.

Katika matokeo yaliyotolewa Jumatatu, mwanafunzi aliyeibuka bora shuleni humo, Boniface Musira alipata alama 412 akifuatwa na Rachel Mutheu 408, Julius Makuu 402 na Timothy Kyalo 400.

“Wanafunzi wanne wamepata alama 400 kwenda juu, 61 wamepata zaidi ya alama 350 na wengine walifanikiwa alama kati ya 324 na 348,” akasema mwalimu mkuu, Bi Janet Malika.

Shule hii ya Siloam Education Centre imo mahala ambapo kuifikia ni kibarua kigumu kutokana na matope, barabara mbaya na misongamano ya watu.

Akiongea na Taifa Leo, Musira, 16 alisimulia alivyojikaza hadi akakabili changamoto nyingi ikiwemo nyumba yao kuporomoka na kuibuka miongoni mwa watahiniwa bora mwaka huu.

Naye Mutheu anasema mamake alimpa moyo na ari ya kusoma na kujituma huku akimwambia asiogope watoto wa kiume: “Mama aliniambia kile mwanamume anaweza kufanya mwanamke pia anaweza kukifanya na pia anaweza kukiboresha zaidi,” akasema Mutheu.

Hapo jana wanafunzi, walimu na wazazi waliimba nyimbo za shangwe pamoja na waliofanya vizuri huku wakiwabeba juu wanafunzi bora.

Karibu na lango la shule, wakazi wa mtaa huo walikuwa wakiajabia matokeo hayo yaliyokuwa kwenye ubao wa matangazo wa shule hii iliyoanzishwa 2013 ikiwa na wanafunzi 30 na sasa ina wanafunzi 3,000.