Habari Mseto

KCPE: Pacha ambao hawajawahi kuachana waapa kutengana hadi waingie sekondari

November 21st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

NA RUTH MBULA

PACHA Beverly na Babra Gichungi ambao wanaopendana sana na ambao mara nyingi huwa pamoja, wameshangaza wengi kwa kuamua kutengana hadi watakapojiunga na shule za upili.

Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE) ni mojawapo za sababu za wasichana hao wawili kutengana ingawa walifikia hilo kabla ya mtihani huo ili kila moja wao awe akijitegemea.

“Tuliamua kwamba ni wakati kila mmoja wetu aishi kivyake. Huu mtihani wa KCPE umetusaidia kuafikia hilo,” akasema Babra anayelenga kujiunga na shule ya upili ya Wasichana ya Pangani huku dakake akilenga Moi High School Kabarak.

Babra, alipata alama 428 naye dadake akakwangura alama 399. Wakati mwanahabari wetu alipowatembelea nyumbani kwao Kisii, Beverly alikuwa akilia machozi kwa uchungu eti alishindwa na dadake.

Wawili hao walio na umri wa miaka 14 na marafiki wakubwa, walikuwa wakilia na kucheka kwa wakati moja baada ya kuyapokea matokeo yao na kuacha mama yao katika njiapanda asijue la kufanya.

“Mama, nimeanguka vibaya, haya si matokeo niliyoyatarajia,” Beverly akaeleza mamake Violet Nyakora akilia.

“Watu wengi walijua dadangu angenishinda na wakamminia sifa kila mara. Lakini nilimwomba Mungu na kutia bidii ili niwathibitishie kwamba hata mimi ningeweza kumbwaga,” akasema Bi Babra huku akikubali kwamba hakuwahi kushinda dadake masomoni awali.

Wawili hao walikuwa wanafunzi wa Shule ya Msingi ya Nyambunwa Academy mjini Suneka, Kaunti ya Kisii.

Mama yao alikuwa na wakati mgumu wa kupongeza Bi Babra na wakati uo huo kumliwaza Bi Beverly.

“Usilie mwanangu, nyinyi nyote mmefanya vizuri kwenye mtihani. Uzuri ni kwamba ushindi huu ni wetu,” akasema Bi Nyakora akiahidi kuwapa ushauri wanawe.