Wanaume hawapendi kufundisha kwenye shule za msingi – Utafiti
Na OUMA WANZALA
IDADI ya wavulana wanaoingia kwenye taaluma ya ualimu inazidi kupungua, huku kazi hiyo ikivutia wasichana zaidi, ripoti ya Baraza la Mitihani ya Kitaifa (KNEC) inasema.
Kulingana na ripoti hiyo, kwa miaka mitano iliyopita kumekuwa na wanafunzi wengi wa kike wanaofanya mitihani ya mafunzo ya ualimu ikilinganishwa na watahiniwa wa kiume.
Mwaka huu, ripoti hiyo inaonyesha kulikuwa na watahiniwa 17,879 wa mitihani ya walimu wa shule za msingi ikilinganishwa na watahiniwa 11,651 wa kiume. Tofauti ni wanafunzi 6,228.
Mwaka uliopita, watahiniwa 13,646 walifanya mtihani huo huku kukiwa na 10,402 pekee wa kiume.
Katika mwaka wa 2016, ripoti hiyo inaonyesha watahiniwa 10,587 wa kike walifanya mtihani huo ikilinganishwa na 8,555 wa kiume.
Mwaka wa 2015 kulikuwepo watahiniwa 10,003 wa kike na 8,656 wa kiume na katika mwaka wa 2014, watahiniwa 9,410 walikuwa wa kike na 7,881 wa kiume.
Mitihani hiyo hutolewa kwa wakufunzi wa ualimu baada ya kozi ya miaka miwili ili kupokea vyeti.
Hii inamaanisha kuwa miongoni mwa walimu zaidi ya 290,000 waliosajiliwa na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC), wengi ni wanawake.
Ripoti hiyo ambayo ilitolewa wiki iliyopita inaonyesha kuwa taasisi za mafunzo ya ualimu za umma zimekuwa zikivutia wanafunzi zaidi kuliko taasisi za kibinafsi.
Hata hivyo, licha ya kuwa na idadi kubw aya wanafunzi, ripoti hiyo inasema watahiniwa wengi hufeli kwenye mitihani yao kila mwaka, ambapo wengi hulazimika kurudia mitihani hiyo.
Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, ni watahiniwa 105 pekee ambao walipata alama bora ya ‘distinction’ kati ya jumla ya watahiniwa 109,079.
Katika mwaka huu kulikuwa na watahiniwa 29,530 ilhali ni 21 pekee ambao walipata alama hiyo, na mwaka uliopita walikuwa watahiniwa watano pekee.
Mwaka huu, watahiniwa 266 walifeli mitihani yao kumaanisha watalazimika kurudia mwaka mzima wa masomo.
Wakati huo huo, wengine 10,457 watahitajika kurudia mitihani mwaka ujao, ikilinganishwa na 12,438 waliofanya hivyo mwaka uliopita.
Hii ni kumaanisha watahiniwa hao watalazimika kusubiri hadi mwaka ujao kufanya mitihani maalumu.
Wizara ya Elimu mwaka huu ilishukisha alama zinazohitajika kwa wanafunzi kujiunga na taasisi za elimu ya walimu kutoka C hadi D+ ili kunufaisha kaunti 17 zinazokumbwa na uhaba mkubwa wa walimu kutokana na changamoto mbalimbali.
Mitihani hiyo hujumuisha masomo 14 ambapo kuna karatasi 21 tofauti za mitihani, mbali na majaribio ya kufundisha darasani.
Takwimu za miaka mitano iliyopita zinaonyesha kuwa mwaka wa 2017 ulikuwa na idadi kubwa zaidi ya watahiniwa waliofeli.