Ukimwi: Maambukizi kwa vijana yanatisha
VERAH OKEYO na ANGELA OKETCH
WATAFITI na wataalamu wa afya wanaadhimisha Siku ya Ukimwi Ulimwenguni hii leo wakitoa wito kwa taifa kuangazia zaidi vijana wachanga, ambao wamekuwa wakichangia pakubwa katika maambukizi mapya ya Ukimwi nchini.
Kiwango cha kitaifa cha maambukizi ya virusi hivyo ni asilimia 7.7, na kuifanya Kenya kuwa miongoni mwa mataifa sita yanayolemewa mno na janga la Ukimwi barani Afrika.
Kulingana na ripoti iliyochapishwa wiki jana na Baraza la Kitaifa la Kudhibiti Ukimwi (NACC), vijana wachanga 17,667 wenye umri wa kati ya miaka 15 na 24 waliambukizwa Virusi vya Ukimwi (HIV). Hii ni asilimia 40 ya maambukizi yote mapya 52,800 yaliyoshuhudiwa nchini Kenya.
Mbali na kuchangia visa viwili kati ya kila vitano vya maambukizi, sababu kuu ya vifo vinavyoshuhudiwa miongoni mwa vijana wachanga ni magonjwa yanayotokana na makali ya Ukimwi.
Ndiyo hali ya kutamausha inayojitokeza hususan ukiongeza matineja walio na umri wa miaka kati ya 10 na 19 katika kundi hilo la vijana wachanga, kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Kiufundi katika NACC, Dkt Celestine Mugambi.
“Matineja wengi na vijana wachanga hawajui hali yao ya HIV. Vilevile, hawana maelezo sahihi kuhusu HIV na Ukimwi,” Dkt Mugambi aliambia Taifa Leo.
Dkt Patrick Oyaro, mtafiti na Afisa Mkuu Mtendaji wa RCTP -Faces, ambalo ni shirika lisilo la kiserikali linaloendesha utafiti wa HIV eneo la magharibi mwa Kenya, alisema ingawa vijana wachanga hupimwa HIV na kupewa matibabu, bado wanakabiliwa na changamoto ya kufuatilia kwa makini taratibu za matibabu.
Alitaja unyanyapaa miongoni mwa vijana hao, hususan shuleni, kama moja ya sababu zinazowafanya kutomeza dawa hizo za kukabiliana na makali ya virusi (ARVs) kwa utaratibu.
Dkt Abdhalah Ziraba, mtaalamu wa afya ya umma katika shirika la
African Population and Health Research Centre (APHRC) alihimiza wadau kuangazia suala la jinsia katika vita dhidi ya Ukimwi akisema juhudi zaidi zinafaa kuelekezwa katika miradi inayowalenga wasichana na wanawake.
Aliandika: “Mengi ya maambukizi yanashuhudiwa katika kundi hili kwa sababu mbalimbali za kijamii.”