• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Lusaka akemea viongozi wanaotaka seneti iondolewe

Lusaka akemea viongozi wanaotaka seneti iondolewe

Na BONIFACE MWANIKI

SPIKA wa Seneti Kenneth Lusaka amewataka Wakenya wasitilie maanani pendekezo la baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaotaka Bunge la Seneti liondolewe kabisa akisema seneti ndiyo asasi ya kipekee iliyosalia inayolinda ugatuzi na kuiondoa itarejesha taifa nyuma kimaendeleo.

Akizungumza wakati wa hafla ya pili ya upigaji mnada wa mbuzi katika kijiji cha Nguni, kaunti ndogo ya Mwingi ya Kati, Kaunti ya Kitui, Bw Lusaka aliisifu seneti kwa kuhakikisha fedha za umma zinazofadhili ugatuzi zinatumika vizuri tena kwenye miradi ya maendeleo inayolengwa.

“Kulikuwa na mfumo wa serikali ya majimbo uliomalizwa mwaka wa 1966 baada ya kuondolewa kwa seneti. Hatuko tayari kurudi enzi hizo kwa kuwa taifa hili tayari limeshuhudia manufaa ya ugatuzi. Bunge la seneti ndilo lililoleta ugatuzi na kuliondoa litakuwa pigo kubwa kwa asasi zinazoendesha serikali hizo,” akasema Bw Lusaka.

Kiongozi huyo pia alimiminia sifa kochokocho Seneta wa Kitui Enoch Wambua kwa kuanzisha hafla za kuwanadi mbuzi akisema hiyo ni njia mojawapo ya kupigana na uchochole ulioota na kukita mizizi katika kaunti hiyo kame na kuimarisha maisha ya wenyeji kupitia ubunifu wa njia za kuwakweza hadi utajiri.

“Nilipokuwa naja hapa niliona kwamba eneo hili limekauka mno na ni kupitia hafla kama hizi ndipo maisha ya wananchi wa Kitui yatakapoimarika. Namwaomba Bw Wambua aendelee kuandaa hafla kama hizi ili kuyaboresha maisha ya watu wa hapa,” akaongeza Bw Lusaka.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mwingi ya Kati, Dkt Gideon Mulyungi alimwomba Rais Uhuru Kenyatta kupendekeza hukumu zaidi kwa maafisa wa umma wanaoshiriki ufisadi ili ‘kamatakamata’ za kila ijumaa zisiishie mzaha mtupu bali maafisa hao washtakiwe na kuhukumiwa vikali mahakamani.

“Iwapo Rais Kenyatta anataka kumaliza kabisa dondandugu la ufisadi nchini basi hana budi ila kuhakikisha wanaokamatwa kwa kushiriki ufisadi wanahukumiwa au kuadhibiwa vizuri la sivyo kukamatwa tu na kufikishwa mahakamani bila kuhukumiwa vikali kutageuza vita hivyo kuwa mzaha mtupu,” akasema Dkt Mulyungi.

Seneta wa Kitui Enoch Wambua naye alisema atahakikisha kwamba wakulima wafugaji wa mbuzi wanaunda vyama vya ushirika ili kuzidisha mapato na kuifanya Kaunti ya Kitui kuwa nambari moja katika mauzo ya nyama ya mbuzi.

.

You can share this post!

Wakataa vinyozi vya Muchomba wakisema ni vya thamani ya...

Wafanyakazi hewa na wasiofika kazini kupokea mishahara hewa

adminleo