Habari Mseto

Tovuti zote za ngono nchini zizimwe – Ezekiel Mutua

December 10th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

NA CHARLES WANYORO

AFISA Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi na Uainishaji wa Filamu nchini Dkt Ezekiel Mutua ameunga mkono wito wa kuzima tovuti zote za filamu za ngono nchini akisema kuwa zinawapa watoto picha zisizofaa na kuzua utovu wa maadili nchini.

Afisa huyo alisema hali tata ya mimba za mapema nchini iliyoshuhudiwa wakati mitihani ya kitaifa ikiendelea ilitokana na watoto kusoma matini ya mapenzi bila kinga na kutazama video za ngono kwa kuwa sekta ya intaneti imeachwa wazi kwa matineja bila udhibiti wowote.

 Dkt Mutua alisema serikali haitaruhusu matini yoyote ambayo inachochea tabia mbovu kwa vijana ambao wanatazamiwa kuwa viongozi wa siku za usoni.

Akihutubu katika ufunguzi wa warsha ya wakufunzi ya Tamasha za Maigizo na Filamu katika Chuo cha Mafunzo ya Kiserikali mjini Embu, afisa huyo alisema kufungwa na kuzuiwa kwa tovuti za ngono ni mojawapo ya suluhu za tatizo hilo.

“Video hizi za ngono zinazopatikana kwa urahisi kwenye mitandao ndizo zinawachochea watoto wetu kufanya ngono kwa umri mdogo. Matini hii ni mbovu na hatari kwa wana wetu. Lazima zizimwe ili kuwakomboa vijana,” akasema.

Aliongeza kuwa mataifa kama Singapore na Milki za Uarabuni zimezuia tovuti za ngono na kudhibiti mitandao yake, na hakuna raia anayeweza kupata ngono mitandaoni kinyume na hapa Kenya ambapo kila mtu anaweza kutazama bila kizuizi.

Alisema kuna uwezekano wa kudhibiti mitandao bila kuingilia haki za watu wazima na kuwalinda watoto ambao wamepagawishwa na video wanazotazama.