• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 4:01 PM
Hofu wafanyabiashara wakilipa wahuni kuua washindani wao

Hofu wafanyabiashara wakilipa wahuni kuua washindani wao

Na NICHOLAS KOMU

WAFANYABIASHARA mjini Nyeri sasa wanatumia magenge ya wahalifu kuhangaisha na kuwaua washindani wao wa kibiashara, polisi wamefichua.

Kukamatwa kwa mfanyabiashara na washukiwa wawili wa ujambazi wikendi iliyopita kumewezesha polisi kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na ongezeko la magenge ya wahalifu wa kukodishwa mjini Nyeri.

Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la visa vya majambazi, wanaosadikiwa kukodishwa, kuvamia biashara mbalimbali mjini Nyeri pamoja na viunga vyake.

Sasa uchunguzi wa polisi umebaini kuwa uvamizi huo ni uhasama unaosababishwa na ushindani wa kibiashara.

Wiki iliyopita, visa vitatu vya ujambazi viliripotiwa katika maeneo ya Ruring’u na Skuta na polisi wanaamini kiini cha uhalifu huo ni ushindani wa kibiashara miongoni mwa wafanyabiashara wa maeneo hayo.

Kulingana na polisi katika visa hivyo vyote, mashambulio yalionekana kama ya kulipiza kisasi.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Nyeri Ali Nuno jana alithibitisha kwamba wanaamini kwamba mfanyabiashara mashuhuri ambaye ametiwa mbaroni, alikodisha majambazi kushambulia mshindani wake wa kibiashara.

“Mwezi huu wa Desemba kulikuwa na visa vitatu vya ujambazi vilivyoripotiwa na maafisa wa upelelezi walipochunguza walibaini kuwa kuna magenge ya majambazi ya kukodisha,” akasema Bw Nuno.

Ijumaa Usiku, mfanyabiashara Patrick Njuguna Maina alikamatwa kutokana na madai kwamba alikodisha majambazi kushambulia mshindani wake wa kibiashara.

Polisi pia walikamata washukiwa wawili; Paul Maingi Nderitu na William Wachira Kariuki wanaodaiwa kutekeleza uvamizi huo.

“Mmoja wao aliwafyatulia polisi risasi mbili na kisha kutupa bunduki yake kichakani. Hata hivyo, alishikwa na sasa polisi wameanzisha operesheni ya kusaka bunduki hiyo. Wanatarajiwa kuikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kuhusika na ujambazi,” akasema mkuu wa polisi.

Mshukiwa wa tatu wa ujambazi anadaiwa kutorokea Nairobi ambapo maafisa wa polisi wanaendelea kumsaka.

Kulingana na polisi, biashara zinazolengwa na majambazi hao ni maeneo ya burudani kama vile baa, ambayo kwa sasa ni kivutio kikubwa wakati wa msimu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya.

Hii si mara ya kwanza kwa visa vya ujambazi kuripotiwa ambapo wamiliki wa biashara wanalengwa na biashara zao kuharibiwa na wahalifu.

Inadaiwa kuwa genge linakodishwa kuanzia Sh5,000 na wafanyabiashara kwenda kuua washindani wao wa kibiashara.

Mara nyingine huvizia njiani mwathiriwa na kisha kumshambulia anapokuwa akirejea nyumbani kutoka kazini.

“Visa vya uhalifu vimepungua kuanzia Agosti, mwaka huu. Lakini uvamizi ambapo wafanyabiashara wanakodisha majambazi kushambulia wenzao ni suala ambalo limetupa wasiwasi,” akasema Bw Nuno.

Washukiwa hao walifikishwa mahakamani jana ambapo walifunguliwa mashtaka ya kuhusika na wizi wa mabavu.

You can share this post!

Walioiba pesa za NHIF wanastahili adhabu ya wauaji, asema...

Wananchi wote walazimishwe kupiga kura ili kuzima ufisadi...

adminleo