Wakazi Nyando walilia msaada kufuatia mafuriko
CECIL ODONGO na RUSHDIE OUDIA
MAKAZI yako hatarini katika Kaunti Ndogo ya Nyando, Kaunti ya Kisumu huku wakazi zaidi ya 300 wakilazimika kuhama baada ya nyumba zao kusombwa na maji ya mafuriko kutokana na mvua kubwa inayoendelea kushuhudiwa eneo hilo.
Maeneo yaliyoathirika pakubwa ni Kano Kabonyo, Ugwe, Kandaria, Kanyagwal, Kakola Ombaka na Ogenya ambapo nyingi za nyumba zilifunikwa na kusombwa kwa mafuriko huku barabara nyingi sasa zikiwa hazipitiki Jamhuri Dei.
Judith Obong’o mkazi wa eneo hilo alisema kwamba mvua hiyo ilianza Jumapili na imekuwa ikendelea kwa kiwango cha kutisha huku ikizua uharibifu mkubwa na kusomba mifugo pia.
Mkazi mwengine Leornard Ogolla, 71 alisimulia jinsi kuku na kondoo wake walivyosombwa na maji ya mafuriko nao ng’ombe aliosalia nao wakikosa malisho kwa kuwa nyasi zimefunikwa kwa maji mengi.
“Sisi wazee ndiyo tumeathirika vibaya kwa sababu hatuwezi kutorokea maeneo salama na pia barabara zinazoelekea hospitalini hazipitiki,” akasema Bw Ogolla.
Chifu wa lokesheni ya Kakola Ombaka Jacob Ongudi jana alisema zaidi ya familia 60 zimelazimika kuhama makwao baada ya nyumba zao kuharibiwa.
“Shughuli zote za kilimo cha mpunga na mahindi sasa zimekwama baada ya kiwango cha maji kuzidi na kufunika mashamba. Kuna hatari ya kutokea kwa mkurupuko wa magonjwa yanayotokana na maji chafu,” akasema Bw Ongudi.
Wakazi hao sasa wanaiomba serikali kuu na ile ya kaunti kuingilia kati na kuwaletea msaada wa vyakula, neti ya kukinga mbu, maji safi ya kunywa, madawa miongoni mwa mahitaji mengine ya kimsingi ili kuwaepushia dhiki ya njaa.
“Tunaomba msaada wa mahitaji muhimu kwa sababu matokeo ya mafuriko kwetu ni njaa kubwa,” akasema Bi Obong’o kutoka Kano Kabonyo.
Kaunti ya Kisumu imekuwa ikikabiliwa na mafuriko kila msimu wa mvua. Maeneo ambayo huathirika mara kwa mara yanapatikana katika maeneo bunge ya Nyando, Nyakach, Kisumu Mashariki na Muhoroni.
Mwezi Aprili na Mei, mafuriko yalisomba vijiji kadhaa na kusababisha ukosefu wa makao kwa mamia ya wenyeji.