Uhuru achangamsha Wakenya kwa mavazi yake ya kijeshi
Na CHARLES WASONGA
WAKENYA wengi jana walishangaa kumuona Rais Uhuru Kenyatta akiwa amevalia mavazi rasmi ya kijeshi alipowasili katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo alipoongoza taifa katika maadhimisho ya 55 ya sherehe ya Siku ya Jamhuri.
Ni mavazi yake rasmi ambayo anapaswa kuvalia nyakati za sherehe za kitaifa kama Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote nchini.
Hata hivyo, jana ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuvalia mavazi kama hayo katika sherehe ya kitaifa tangu alipoingia mamlakani mnamo 2013 japo amewahi kuvalia magwanda ya kijeshi katika hafla mbalimbali za Jeshi la Ulinzi (KDF).
Rais Kenyatta alivalia mavazi rasmi ya kijeshi kwa mara ya kwanza mnamo 2014 alipohudhuria shughuli moja ya kijeshi katika eneo la Archer’s Post katika kaunti ya Samburu.
Mwaka huo huo, alivalia sare hizo wakati wa Sherehe za KDF zilizoandaliwa katika Chuo Cha Mafunzo ya Kijeshi Lanet, kaunti ya Nakuru na wakati wa maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Kikosi cha Jeshi la Wanamaji jijini Mombasa.
Kwa mara nyingine Rais Kenyatta alivalia mavazi ya kijeshi katika Sherehe ya Kufuzu kwa Polisi wa kupambanana na fujo (GSU) katika chuo cha Mafunzo ya kikosi hicho kilichoko Embakasi, Nairobi.
Jana, Rais alilakiwa kwa furaha na bashasha alipowasili katika uwanja wa Nyayo akiwa amevalia mavazi hayo rasmi ya kijeshi huku akibeba upanga kwenye mkono wake wa kushoto.
Akihutubu kabla ya kumwalika Rais Kenyatta, Naibu Rais William Ruto alifafanua kuwa kiongozi wa taifa alivalia mavazi rasmi ya kijeshi kwa sababu “yeye pia ni amiri jeshi mkuu wa majeshi yote nchini.”
“Kando na kuwa rais wa nchi na kiongozi wa taifa, Rais pia ni Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi yote nchini nah ii ndio maana leo amevalia mavazi yake rasmi ya kijeshi,” akaeleza.
Rais mstaafu Daniel Moi pia waliwahi kuvalia mavazi ya kijeshi katika sherehe za kitaifa au zile za kijeshi.
Hata hvyo, Rais wa tatu nchini Mwai Kibaki, hakuwahi kuvalia mavazi ya kijeshi hadharani katika kipindi cha uongozi wake kilichodumu kwa miaka 10