Habari Mseto

Jinsi babake Raila alinisaidia nisifukuzwe chuoni – Moses Kuria

January 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WANDERI KAMAU

WAZIRI wa Utumishi wa Umma, Moses Kuria, ameeleza jinsi marehemu Jaramogi Oginga Odinga alivyomsaidia kumaliza masomo yake katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Jaramogi ni babake kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, na alifariki mnamo Januari 20, 1994.

Mnamo Jumapili, Bw Kuria alieleza jinsi agizo la Jaramogi kwa marehemu Otieno Kajwang’ lilivyowaokoa dhidi ya kufukuzwa kutoka chuo, kwa madai ya kuwaongoza wanafunzi kushiriki kwenye mgomo.

“Siku ambayo tulikuwa tufukuzwe chuoni kwa madai ya kuwaongoza wanafunzi kushiriki kwenye mgomo, marehemu Jaramogi alimwagiza wakili Otieno Kajwang’ (aliyehudumu baadaye kama Seneta wa Homa Bay) kufika mahakamani na kuwasilisha ombi la kupinga uamuzi huo. Bw Kajwang’ aliamka mapema sana na kuwasilisha ombi hilo. Hilo ndilo lililotupa nafasi ya kujitetea chuoni na maombi yetu kukubaliwa. Ikiwa Jaramogi hangefanya hivyo, huenda hatungemaliza masomo yetu,” akasema Bw Kuria, kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni.

Soma pia Mjumbe wa Kiuchumi wa Amerika akataa kukutana na Moses Kuria kwa sababu ya ‘mdomo mchafu’

Halafu Naondoka Wizara ya Biashara baada ya kufufua uzalishaji wa viwanda, asema Kuria

Bw Kuria alikuwa kiongozi wa wanafunzi pamoja na wanasiasa kama vile mbunge wa zamani wa Mukurwe-ini, Kabando wa Kabando.

Waziri huyo alitaja hilo kama sababu kuu ambapo amekuwa akihudhuria makumbusho ya Jaramogi kila Januari 20.

“Nilihudhuria makumbusho ya kwanza mnamo 1995. Kando na makumbusho hayo, nilikuwa pia miongoni mwa watu kadhaa kutoka eneo la Kati waliohudhuria mazishi ya Jaramogi na hata kujaribu kubuni mwafaka wa kisiasa baina ya jamii za Agikuyu na Waluo, ijapokuwa juhudi hizo hazikufua dafu,” akasema Bw Kuria.

Waziri huyo alitaja hilo kama sababu kuu ya kuhudhuria makumbusho ya kiongozi huyo, licha ya kuwa katika mrengo tawala wa Kenya Kwanza.

“Mimi ni mwanafunzi wa historia. Siwezi kusahau mahali marehemu [Jaramogi] aliponitoa. Hata ikiwa tumekuwa na tofauti za kisiasa na Bw Odinga na viongozi wengine nchini, hilo halifai kufuta safari yetu ya kisiasa tuliyotembea pamoja,” akasema Bw Kuria.

Waziri huyo alizua maswali kutokana na uwepo wake katika makumbusho hayo, ikizingatiwa amekuwa miongoni mwa wakosoaji wakuu wa Bw Odinga.