• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Mmiliki wa kampuni ya juisi ya Afia kujitosa kwa soko la hisa

Mmiliki wa kampuni ya juisi ya Afia kujitosa kwa soko la hisa

MARY WAMBUI na PETER MBURU

Mmiliki wa kampuni ya Kevian Kenya ambayo hutengeneza vinywaji kama Afia na vingine, Kimni Rugendo amedokeza kuwa kampuni hiyo sasa huenda ikaorodheshwa katika soko la hisa la NSE, hali ambayo itawafanya Wakenya kununua hisa za kampuni hiyo.

Hali hii ni ishara ya kubadilishwa kwa usimamizi ambako kunatarajiwa, na Bw Rugendo alisema “Tutawataka watu kujiunga na umiliki hizi karibuni, muwe tayari.”

Hata hivyo, Bw Rugendo hakueleza wazi wakati kampuni hiyo inatarajiwa kuorodheshwa katika soko hilo la hisa, kwani mpango bado uko katika hatua za awali.

Alifanya tangazo hilo baada ya kuzindua ushirikiano na kampuni ya kutengeneza vinywaji kutoka Uingereza ‘Vimto’, ambao utaifanya kampuni ya Kevian kutengeneza vinywaji vya Vimto humu nchini.

Biashara hiyo ya kifamilia ambayo ilianza mnamo 1991 na utengenezji wa maji ya chupa, kisha juisi za matunda, na vyakula miaka ya awali karne hii katika matawi yake ya Thika na Nairobi imekuwa ikizidi kukua miaka hiyo yote.

Hali hiyo imeiwezesha kukua, kiwango cha kupata mkopo wa Sh3bilioni kutoka kwa shirika la kimataifa.

Wanawe Bw Rugendo wawili wanafanya kazi katika kampuni hiyo.

Kampuni ya Kevian imeajiri watu 800 moja kwa moja, kando na maelfu ya wakulima ambao husambaza matunda kwake na kwa ushirikiano mpya na kampuni ya Vimto itaajiri watu 500 zaidi katika kazi za mauzo na kusambaza bidhaa.

You can share this post!

Gor wachupa kileleni KPL

Kaunti yageukia soka kunasua vijana kutokana na minyororo...

adminleo