ANGLO LEASING: Polisi aamriwa kutoa ushahidi
Na RICHARD MUNGUTI
HAKIMU mwandamizi Bi Martha Mutuku Jumatatu alimwamuru afisa mkuu wa Polisi aliyepokea ushahidi katika kashfa ya Sh43bilioni ya Anglo-Leasing afike kortini Jumanne kutoa ushahidi.
Bi Mutuku alitoa agizo hilo baada ya kuombwa na wakili Kioko Kilukumi anayewatetea ndugu wawili na baba yaw a jamii ya Kamani (walio kizimbani) aamuru Bw Gedion Rukaria afike kortini kuhojiwa.
“Naomba hii mahakama iamuru Bw Rukaria afike kortini kutoa ushahidi,” alisema Bw Kilukumi.
Wakili huyo anayewatetea Deepak Kamani ( anayesimama pichani) , Chamnilal Kamani (anayeketi) na waliokuwa makatibu wakuu David Onyonka na Dave Mwangi alisema “ ushahidi wa Bw Rukaria ni muhimu hasa ikitiliwa maanani mahakama kuu iliamuru akamilishe kutoa ushuhuda wake kortini.”
Mahakama ilielezwa afisa huyo wa polisi anahudumu katika kaunti ya Machakos.
“Naamuru Bw Rukaria afike kortini tarehe kumi na moja mwezi Desemba saa tano kutoa ushahidi na kuhojiwa na mawakili wanaowatetea washtakiwa.”