• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
Chokoraa waondolewa Muthurwa

Chokoraa waondolewa Muthurwa

Na SAMMY KIMATU

WATOTO zaidi ya kumi wa kurandaranda mitaani walikamatwa Ijumaa subuhi katika msako wa kuwaondoa kutoka katikati ya jiji ambapo msako huu unaendeshwa katika wiki ya pili mfululizo.

Operesheni hiyo inafanywa na maafisa wa Kaunti ya Nairobi wakishirikiana na maafisa wa polisi.

Katika tukio la jana, watoto hao, wote wakiwa ni wavulana, walivamiwa wakiwa wamelala chini ya kivukio cha Soko la Muthurwa/ Barabara ya Haile Selassie mwendo wa saa tatu za asubuhi.

Naibu Mkurugenzi wa Operesheni wa Serikali ya Kaunti, Bw William Kangogo alithibitisha kisa hicho na kusema kwamba watoto hao walipelekwa katika kituo cha watoto cha kurekebisha tabia kilichoko Mashariki mwa jiji la Nairobi.

“Nia ya kaunti ni kuwa na mazingira masafi jijini na kuhakikisha usalama wa watu ni shwari mjini. Watoto tunaokamata na ni wachanga na hasa wasichana hupelekwa mtaani Kayole, na wale wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 21 hupelekwa katika eneo la Joseph Kang’ethe mtaani wa mabanda wa Kibera tofauti na wale wakongwe ambao hupelekwa katika Mji wa Huruma ulioko maeneo ya Runda,” Bw Kangogo akadokeza.

Aliongeza kwamba tangu msako huo uanze, kumeripotiwa kushuka kwa idadi wa watoto hao licha ya changamoto zilizopo.

Alisema sababu kuu ya kupatikana kwa watoto hao jijini ni kwa sababu wanakaa bure na likizo ya Disemba imekuwa ndefu tangu shule zifungwe mwezi Oktoba.

“Watoto hawa hutoka mitaani ya mabanda ya Kibera, Mathare na  Mukuru baada ya kushawishiwa na wengine,” Bw Kangogo akasema.

Kwenye eneo la kisa, kulikuwa na magunia, makaratasi, katoni , nguo kuukuu, nyaya za magurudumu ya magari na kinyesi na mkojo huku ukuta ukuta wa mawe ukiwa mweusi tititi kutokana na moshi ufukao wakiwa wamewasha moto ndio taswira iliyoshuhudiwa.

You can share this post!

Kizaazaa muuaji wa marehemu kujitokeza mazishini

Kenya yaiondoa Zambia Copa Coca-cola U-16

adminleo