Uhuru na Raila washauriana kisiri usiku
Na WAANDISHI WETU
RAIS Uhuru Kenyatta alikutana kisiri na kiongozi wa ODM Raila Odinga mnamo Alhamisi usiku katika Ikulu ndogo ya Kisumu bila wandani wao.
Baada ya msururu wa mikutano ya hadhara Alhamisi, Rais Kenyatta kwanza alikutana na viongozi wa Luo Nyanza katika Ikulu ya Kisumu kabla baadaye kukutana na Bw Odinga wakiwa wawili.
Taifa Leo haikubaini ajenda ya mkutano kati ya Rais Kenyatta na viongozi wa Luo Nyanza ambao ulikuwa na usiri mkubwa kwani hata viongozi kutoka Kisii waliokuwepo waliagizwa kuondoka.
Gavana wa Kisii James Ongwae, na mwenzake wa Nyamira John Nyagarama pamoja na mbunge wa Kitutu Chache Kaskazini Jimmy Angwenyi waliombwa kuondoka katika mkutano huo uliohusisha magavana, wabunge na maseneta wa Luo Nyanza.
Hata hivyo, baadaye Rais Kenyatta vilevile alikutana na viongozi hao wa Kisii.
Seneta wa Siaya James Orengo na Kiongozi wa walio wachache Bungeni John Mbadi walisema Rais Kenyatta na Bw Odinga walitaka kukutana na viongozi wa Luo Nyanza pekee.
“Mnatakiwa muondoke kwa heshima kwani Rais angependa kukutana na viongozi wa Luo Nyanza, bila hata MCAs,” Bw Orengo alinukuliwa akisema.
Naye Mbadi akaongeza: “Ni ombi kwa heshima tu, Rais atakutana na kila mtu baadaye.” Naibu Rais William Ruto ambaye alikuwa ameandamana na Rais katika ziara hiyo ya siku mbili hakudhuria kikao hicho cha Ikulu ya Kisumu.
Gavana wa Migori Okoth Obado vilevile hakuhudhuria kikao hicho.
Baada ya mikutano na viongozi hao, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Oburu Odinga alifichua kuwa Rais Kenyatta baadaye alikutana na Bw Odinga faraghani kwa muda.
“Baadhi ya mambo ambayo walizungumzia ni mpango wa kuwafidia waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2017,” Bw Oburu aliambia kituo cha radio cha Ramogi katika mahojiano.
Jana asubuhi, Bw Odinga pamoja na mkewe Ida Odinga walimwandalia Rais Kenyatta kiamsha kinywa nyumbani kwao Bondo,
Baadaye, wawili hao walitunukiwa shahada za uzamifu (PHD) za heshima kutokana na hatua yao ya kukomesha uhasama wa kisiasa na kuamua kufanya kazi pamoja.
Walitunukiwa heshima hiyo na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia ya Jaramogi Oginga Odinga (JOOUST) wakati wa sherehe ya mahafala mjini Bondo, Kaunti ya Siaya.
Wakihutubu baada ya kutunikiwa shahada hizo, viongozi hao waliapa kuhakikisha muafaka waliotia saini mnamo Machi 9 unazaa matunda ambayo yatawafaidi Wakenya wote.
“Nitajitolea kuendelea kufanya kazi na ndugu yangu Raila na Wakenya wote ili kujenga nchi yenye usalama, umoja na maafanikio kwa manufaa ya wote,” Rais akasema.
Bw Odinga alisema salamu yao nje ya Jumba la Harambee ilionyesha “kujitolea kwetu kama taifa kujifunza kutokana na makosa ya zamani ili kujiandaa kwa ufanisi.”
“Kama taifa, hatupaswi kukubali kugawanywa tena na siasa au chuki za kikabila,” kiongozi huyo wa chama cha ODM akasema.
Baadaye jana jioni, Rais Kenyatta alifufuliza hadi kaburi la babake Raila, hayati mzee Jaramogi Oginga Odinga ambapo aliweka shada la maua. Rais vilevile aliweka maua katika kaburi la Fidel Odinga, mwanawe, Raila.
“Tunataka kuishi vile Mzee Kenyatta na Mzee Jaramogi walikuwa wakiishi, kwa kuleta jamii zetu pamoja,”Rais Kenyatta aliambia jamaa za Bw Odinga.