Madiwani wamkejeli Raila kutaka idadi yao ipunguzwe
NA ERIC MATARA
PENDEKEZO la kiongozi wa chama cha ODM Bw Raila Odinga la kupunguza idadi ya madiwani nchini ili kupunguza mzigo wa malipo umewaudhi baadhi ya madiwani Kaunti ya Nakuru.
Zaidi ya madiwani 10 walioongozwa na diwani wa wadi ya Kabazi Dkt Peter Mbae, jana walikejeli tamko la kiongozi huyo na kuwataka viongozi wengine kukoma kudhalilisha majukumu ya madiwani nchini.
“Viongozi wanafaa kukoma kutudunisha. Sisi ni viongozi muhimu sana katika kuwaunganisha watu na serikali kuu. Tunatangamana na wananchi wa kawaida kila siku na tunahusika pakubwa kuwaletea maendeleo,” akasema Dkt Mbae.
Aliongeza kuwa wanamheshimu Bw Odinga lakini wakakosoa pendekezo lake, wakisema halifai.
“Badala ya kuwazia kupunguza idadi ya madiwani, viongozi wanafaa kuungana kuhakikisha tunalipwa vizuri. Tunafaa kupokea mishahara minono kwa kuwa sisi ndio kiunganishi cha wananchi na serikali kuu,” akasema.
Bw Odinga ambaye alihutubu katika Kaunti ya Homa Bay Jumamosi katika sherehe ya kumkaribisha nyumbani mbunge wa Rangwe Lillian Gogo, alisema taifa hili limelemewa na mzigo wa malipo ya madiwani ambao hupokea mamilioni kila mwezi.
Pia aliwaonya dhidi ya kupigana bungeni na badala yake kutumia nguvu hizo katika uboreshaji wa huduma.
Alisema kupunguzwa kwa idadi ya wadi kunafaa kuwa katika marekebisho yanayopendekezwa ya katiba huku naye Dkt Mbae akisema visa vichache vya utovu wa nidhamu wa baadhi ya madiwani havifai kuzua mjadala wa idadi ya wadi kupunguzwa.