Habari Mseto

Krismasi ya mapema kampuni ya magari ikiwapuguzia wateja bei

December 17th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

NA FAUSTINE NGILA

WAFANYABIASHARA na kampuni kadhaa nchini wana kila sababu ya kutabasamu baada ya kampuni moja kuwapunguzia bei ya ununuzi na ukodishaji wa magari katika hafla iliyofanyika mjini Naivasha.

Kampuni ya Quipbank Trust Limited ikishirikiana na Vehicle and Equipment  Leasing Limited (Vaell) imepunguza bei ya magari zaidi ya 450 katika msimu huu wa Krismasi kwa zaidi ya asilimia 50.

Wateja walionyesha furaha yao baada ya magari hayo ambayo awali yaliuzwa kwa kati ya Sh5 milioni na Sh10 milioni sasa kuuzwa kwa kati ya Sh2 milioni na Sh4 milioni.

Mteja mmoja ambaye ni afisa wa huduma wa mojawapo ya kampuni zilizofaidika, KOBO Safaris, Bi Helen Nduta alisema alipendezwa na jinsi wateja walikubaliwa kukagua magari kabla ya kuyalipia na kutaja mchakato huo kuwa laini.

Kutoka kushoto: Afisa mkuu wa huduma katika kampuni ya KOBO Safaris, Bi Helen Nduta, mkurugenzi wa biashara wa Quipbank Bw John Mogire na meneja wa mauzo wa kampuni hiyo Bw Philip Nyandieka walipohutubia wanahabari. Picha/ Faustine Ngila

“Magari haya yako katika hali bora ya huduma na yatarahisisha kazi yetu msimu huu wa Krismasi. Tunalenga kununua magari zaidi. Magari ya Toyota Landcruiser yanaweza kuhimili barabara mbovu na kupita kwa matope wakati wa mvua,” akasema.

Mkurugenzi wa biashara wa Quipbank, Bw John Mogire alisema kwamba kampuni hiyo inajizatiti kutoa magari zaidi kwa ajili ya mauzo na ukodishaji kuwafaa wateja.

“Kila mteja ana mahitaji tofauti. Tuna magari tofauti kwa mahitaji tofauti kumfa kila mteja huku tukiwazia kuanza kuwapa magari mapya kutosheleza mahitaji yao,” akasema.