• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Mlima Kenya tayari kumnasa Mudavadi

Mlima Kenya tayari kumnasa Mudavadi

Na LEONARD ONYANGO

WANASIASA kutoka Mlima Kenya wameonyesha dalili za kuanza juhudi za kumwinda kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi huku wakimtaka kuunga mkono muafaka baina ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Ujumbe wa wanasiasa wa Mlima Kenya waliobwagwa katika uchaguzi uliopita, wakiongozwa na aliyekuwa naibu spika wa Bunge la Kitaifa Kembi Gitura na aliyekuwa seneta wa Nyeri Mutahi Kagwe Jumatatu walimtembelea Bw Mudavadi nyumbani kwake katika mtaa wa Riverside, Nairobi, ambapo walimshawishi kuunga mkono pendekezo la kurekebisha katiba.

Rais Uhuru Kenyatta alipokuwa jijini Kisumu wakati wa hafla ya uzinduzi wa Huduma ya Afya kwa Wote kwa gharama nafuu (UHC), alidokeza kwamba kuna haja ya kufanyia mageuzi mfumo wa utawala nchini kwa kupanua serikali.

Ili serikali ipanuliwe na kubuni nyadhifa zaidi kama vile waziri mkuu ni sharti katiba ibadilishwe kupitia kura ya maoni.

Licha ya kusisitiza kuwa mkutano wa jana ulikuwa wa maakuli ya mchana kusherekea Krismasi, Bw Mudavadi alifichua kuwa walijadili suala la kura ya maamuzi na kupambana na ufisadi.

“Mkutano huu haufai kupuuzwa kwani tulijadili mambo muhimu yakiwemo kura ya maamuzi, uchumi, jinsi ya kukabiliana na ufisadi kati ya masuala mengineyo ya kitaifa,” Bw Mudavadi akasema baada ya kufanya kikao cha faragha na wanasiasa hao kwa takribani saa tano.

Bw Mudavadi alisema kuwa anakubaliana na marekebisho ya katiba lakini kuna haja ya kujadili kwa kina vipengele vinavyofaa kubadilishwa.

Mwezi uliopita, Naibu Mwenyekiti wa chama cha Jubilee ambaye ni mwandani wa Rais Kenyatta, Bw David Murathe, alikutana kisiri na Bw Mudavadi nyumbani kwake katika eneobunge la Gatanga, Murang’a; hatua iliyozua minong’ono ya kuwa kiongozi huyo wa ANC alishawishiwa kupewa wadhifa serikalini na kuunga mkono muafaka baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Bw Mudavadi amekuwa akikosoa muafaka huo akisema kuwa haukuhusisha viongozi wote.

Kiongozi wa ANC pia amekuwa akishutumu vinara wenzake wa NASA; Bw Odinga na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kwa kuwataja kama ‘wasaliti’ kutokana na hatua yao ya kukubali kushirikiana na Rais Kenyatta. Bw Mudavadi pia ameshikilia kuwa hatakubali kuchukua wadhifa wowote kutoka kwa Rais Kenyatta.

“Tulijadili mabadiliko ya Katiba lakini wala si siasa za 2022. Vilevile, tunaunga mkono muafaka baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga,” akasema Bw Kagwe.

Waziri huyo wa zamani wa Mawasiliano, alisema kuwa viongozi wa Mlima Kenya wataendelea kufanya mikutano zaidi na Bw Mudavadi “kujadili masuala yenye umuhimu wa kitaifa”.

Kikao cha jana kinajiri siku mbili tu baada ya viongozi hao kutoka Mlima Kenya kukutana na naibu mwenyekiti wa ODM aliye Gavana wa Kakamega, Bw Wycliffe Oparanya.

You can share this post!

Aibu ya mwaka Asante Kotoko ya Ghana kuiba taulo za hoteli...

Nyanya, 76 afariki baada ya kukosa kumtumbuiza Rais Kisumu

adminleo