• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
Mikakati ya  kumaliza kero la uhalifu Mombasa

Mikakati ya kumaliza kero la uhalifu Mombasa

MOHAMED AHMED Na WACHIRA MWANGI

VIONGOZI wa kisiasa na maafisa wa usalama Kaunti ya Mombasa, wamechukua hatua za kukomesha mauaji ambayo yameongezeka hasa maeneo ya Nyali na Mombasa.

Wakiongozwa na Gavana Hassan Joho na mshirikishi wa eneo la pwani Benard Leparmai, viongozi hao walikubaliana kuwa, kuna haja ya kuhusisha jamii katika vita dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya ambazo zimehusishwa na ongezeko la uhalifu.

Kwenye maazimio yaliyosomwa na Naibu Kamishna wa Nyali Gitonga Marete baada ya mkutano wa viongozi na kamati ya usalama, bunge la kaunti ya Mombasa litapitisha sheria kila mtaa wa nyumba za makazi uwekwe taa za usalama ambazo zitakuwa lazima ziwashwe kila usiku.

Viongozi hao pia walikubaliana kuwa taa za barabarani ziwekwe Mombasa na wakazi wakahimizwa waweke kamera za usalama pamoja na kutumia teknolojia ya kisasa ya kuimarisha usalama.

“Pia, tumekubaliana kuwa viongozi wote watakumbatia ushirikiano, watashauriana na kila mmoja,” alisema Bw Marete.

Maafisa wa usalama pia walikosolewa na kutakiwa kudumisha maadili na uwazi katika utekelezaji wa operesheni zao. Wadau wote na umma walitakiwa kutoa habari zitakazosaidia kukabiliana na uhalifu.

Viongozi hao walisema juhudi za pamoja zinahitajika kudhibiti vilabu vya usiku na kuchunguza upya utoaji wa leseni za kuuza pombe Kaunti ya Mombasa.“Tumekubaliana kuwa tutaanzisha mpango wa “Vijana Kwa Vijana” mashinani. Kutakuwa na doria za mara kwa mara za polisi waliovalia kiraia ili waweze kukabiliana na uhalifu,” alisema.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na wabunge wote sita wa Mombasa, madiwani, viongozi wa kidini na mashirika ya kijamii, serikali ya kaunti na wabunge watashauriana ili kuanzisha mipango ya kuimarisha usalama kama vile kujenga vituo vya polisi na kuweka taa za usalama. “Kutabuniwa nafasi za kuwasaidia wanaotaka kurekebishwa au wale wanaoonyesha dalili za kubadilisha maisha yao,” alieleza Bw Marete.

Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo uliochukua saa mbili katika taasisi ya mafunzo ya serikali ni kamishna wa kaunti Evans Achoki, Seneta Mohammed Faki, wabunge Mohamed Ali (Nyali), Ali Mbogo (Kisauni), Badi Twalib (Jomvu), Mishi Mboko (Likoni), Abdulswamad Nassir (Mvita) na Omar Mwinyi (Changamwe) miongoni mwa wengine.

Viongozi hao waliamua kwamba watakuwa wakiandaa mikutano kama wa jana kila baada ya miezi mitatu. Waliamua kuzika tofauti zao ili kukabiliana na tatizo la ukosefu wa usalama ambalo limekuwa kero kwa wakazi wa kaunti hiyo.Kabla ya mkutano wa jana, viongozi wa kisiasa na maafisa wa usalama walikuwa wakilaumiana lakini jana, waliamua kushirikiana ili kukomesha uhalifu.

Mkutano huo ulikuwa wa kwanza tangu wimbi la mauaji lizuke Nyali na Kisauni ambako zaidi ya watu 20 wameuawa. “Tunafaa kuacha kulaumiana na kuanza kushauriana, hii ndiyo dhamira ya mkutano huu na kama viongozi ni jukumu letu kuhakikisha tuna amani na uthabiti kwa kufanya hivi tunafaa kuungana,” Bw Joho alisema kabla ya mkutano.

You can share this post!

Asingizia ulevi baada ya kuwaua mabinti wake wawili

Hatutaki minofu, tunataka pombe, wazee wafoka

adminleo