• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 PM
NGILA: Wizara itumie teknolojia za kisasa kumaliza njaa nchini

NGILA: Wizara itumie teknolojia za kisasa kumaliza njaa nchini

 NA FAUSTINE NGILA

WIKI iliyopita kampuni ya utafiti wa kompyuta ya IBM ilishirikiana na kampuni ibuka ya teknlolojia ya kilimo ya Hello Tractor kuzindua jukwaa la mtandaoni ili kuwapa wakulima wadogo wadogo taarifa kuhusu mbinu za kuimarisha mavuno.

Hatua hii inajiri wakati mwafaka, hasa ikizingatiwa serikali imeorodhesha utoshelevu wa chakula kwenye mpango wake wa Ajenda Nne Kuu, na sasa wavumbuzi wamejizatiti kuibua teknolojia za kupiga jeki mpango huo.

Kwenye hafla ya uzinduzi, naibu mkuu wa IBM Research Africa Bwe Solomon Assefa alielezea kuwa ushirikiano huo utaleta jukwaa linalowaunganisha wanabenki, wakulima na kampuni za trakta ili kuboresha ufadhili na utumizi wa mashine kuongezea mavuno na mapato.

Hatua hii ni muhimu na inafaa kupongezwa, lakini swali kwa akili za wapenzi wa teknolojia ni, Je, mbona serikali haionekani popote katika juhudi za kiteknolojia za kuimarisha kilimo?

Serikali inafaa kuchangia, kwa mawazo, miundombinu au ufadhili wa kifedha katika mambo ambayo yanailetea taifa hili fahari.

Yamkini serikali ya Kenya imeachwa nyuma katika masuala ya kiteknolojia, na sababu kuu ni kuwa hakuna kituo cha utafiti wa kiteknolojia cha serikali kuhusu matatizo yanayokumba nchi hii.

Licha ya kuwa na vijana wapenzi wa teknolojia na ubunifu, hakuna mafunzo ya kukuza talanta hizi.

Kile ambacho serikali inaweza kufanya labda ni kuelimisha Wakenya kuhusu malengo yake ya kutokomeza baa la njaa nchini, na mbinu itakayotumia.

Kwa mfano, IBM na Hello Tractor zinatumia teknolojia za Blockchain, jukwaa la kilimo na intaneti kwa pamoja ili kuboresha mawasiliano kati ya benki, trakta, wakulima na wauzaji wa vifaa vya kilimo.

Serikali inafaa kutumia asasi zake za kukusanya na kuchanganua data kuwapa taarifa muhimu wakulima ili kuwawezesha kujua mbegu na dawa zinazofaa kwa maeneo mbalimbali, wakati wa kupalilia, fatalaiza inayofaa na mimea inayoweza kukuzwa kwa maeneo yao.

Iwapo Wizara ya Kilimo itakuja na jukwaa la mtandaoni ambapo litawashauri wakulima kuhusu utabiri wa hali ya hewa, jinsi ya kutunza mimea mbalimbali, mashine mwafaka na soko la hakika la mavuno, basi ajenda ya chakula kwa wote litaafikiwa.

Lakini ikizidi kutegemea wavumbuzi wa kujitegemea katika vita dhidi ya makali ya njaa, basi haitapiga hatua ya maana katika kutia baa la njaa kwa kaburi la sahau.

You can share this post!

Hatutaki minofu, tunataka pombe, wazee wafoka

ONYANGO: Visa vya polisi kujiua vichunguzwe kwa kina

adminleo