Kifo cha Kendereni: Kindiki asema polisi hawakumuua mshukiwa wa ulanguzi
NA WINNIE ATIENO
SERIKALI imekanusha madai kwamba ilihusika katika mauaji ya mshukiwa wa ulanguzi wa dawa za kulevya Swaleh Yusuf Ahmed, ambaye pia alikuwa akifahamika kama Kendereni.
Inadaiwa Kendereni alikuwa akiendesha shughuli za ulanguzi eneo la Pwani baada ya kifo cha Ibrahim Akasha mnamo 2000.
Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki amedokeza huenda mshukiwa huyo wa ulanguzi aliuawa na washindani wake.
Vyombo vya usalama vinashuku kuwa Swaleh ndiye alikuwa mlanguzi mkuu wa mwisho, aliyehakikisha kuwa eneo la Pwani lilikuwa na usambazaji wa dawa za kulevya kila uchao.
Mlanguzi huyo aliyeuawa alichukuliwa katika nyumba yake eneo la Kikambala mnamo Machi 8 saa mbili jioni, na watu ambao baadaye wangemuua na kuutupa mwili wake uliogunduliwa katika kichaka kilomita kadhaa kutoka nyumbani kwake eneo la Kuruwitu, kaunti ya Kilifi mnamo Machi 16.
Wakati wa kifo chake,Swaleh alikuwa akikabidhiwa na madai kadhaa yanayohusika na operesheni za ulanguzi wa dawa za kulevya yenye thamani ya mailioni ya fedha. Yeye pamoja na mkewe Asma Abdalla Mohamed, walikuwa wamehusishwa na ulanguzi huo.
Polisi walikuwa wamefyata mdomo kuhusu suala hilo. Licha ya hayo, Bw Kindiki amelaumu biashara hiyo isiyo halali kwa kifo chake.
Alizikwa mnamo Machi 17 katika makaburi ya Sargoi jijini Mombasa katikati ya urugu zilizolazimu vyombo vya usalama kuwatuma maafisa wengi wa polisi kutuliza hali.
“Baadhi ya magenge ya kihalifu, hushindana na hata kuumizana. Kwa hivyo hatuwezi sema,” akasema waziri huyo wakati wa ziara katika kituo cha kuwarekebisha walioathirika na dawa za kulevya katika eneo la Miritini.
Aidha, wakuu wa idara ya polisi katika eneo la Pwani waliambia Taifa Leo kuwa mshukiwa huyo aliuawa na mahasidi wake.
“Bado tunachunguza ila polisi hawakuhusika. Ulimwengu wa ulanguzi huwa hatari sana kwa sababu ya uhalifu unaoendelea humo. Huwa wanaangamizana wenyewe kwa wenyewe kila biashara inapokwenda kombo. Tunafanya uchunguzi zaidi kubaini ni nani aliyemuua,” akasema mmojawapo wa polisi wakuu katika eneo la Pwani ambaye aliomba kutotajwa.
Prof Kindiki alitetea idara ya usalama akisema kuwa wao hutekeleza shughuli zao kwa kufuata sheria.
Aliongeza kuwa polisi walikuwa wamepewa mwongozo kutumia nguvu zote kisheria kuwakamata na kutuliza athari zote za usalama wa taifa ikiwemo ugaidi na ulanguzi.