Sonko abomoa vyoo, atisha kubomoa hoteli ya Marble Arch
Na MWANDISHI WETU
GAVANA wa Nairobi Mike Sonko Ijumaa alitisha kubomoa hoteli ya Marble Arch inayomilikiwa bilionea Mike Maina kwa kuiweka alama, baada ya kuapa Alhamisi.
Alhamisi, gavana huyo alibomoa vyoo vya kutumiwa na umma ambavyo vinamilikiwa na mfanyabiashara huyo, baada ya kudai kuwa anatumia hati feki za umiliki wa shamba kuwatimua watu, alipopokea amri kutoka kwa korti.
Bw Sonko alidai kuwa Bw Maina ndiye amesababisha ubomoaji wa nyumba mtaa wa Kayole, ambao umeacha familia nyingi bila makao. Katika video ambayo gavana huyo alikuwa akimpigia simu Bw Maina, alitumia lugha chafu na ya matusi, akimzomea kuwa alitumia hati feki za umiliki wa ardhi kuihadaa mahakama na kuifanya kumpa amri za kuwatimua wakazi fulani wa mtaa wa Kayole.
Eneo la kuegesha magari na vyoo vya umma vilivyo karibu na hoteli hiyo vinasemekana kuwa katika ardhi ya umma, ambayo inamilikiwa na idara ya uzima moto ya serikali ya kaunti ya Nairobi.
Hatua ya gavana huyo ilikuja siku moja tu baada ya serikali kusimamisha visa vyote vya ubomoaji nchini.
Lakini akimjibu Gavana Sonko, Bw Maina alisema kuwa hajanyakua ardhi yoyote.
“Nina hati halali za umiliki wa shamba na ni uchungu sana kunitusi na kuninyanyasa mimi kama mwekezaji nisiye na makossa. Badala yake, Sonko angekuja pale na kunipa magizo ya Rais, ambayo ningeheshimu.”