Habari Mseto

Sherehekeeni Krismasi bila wasiwasi, Boinnet awahakikishia Wakenya usalama

December 22nd, 2018 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

INSPEKTA Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet amewahakikishia Wakenya kwamba usalama umeimarisha kote nchini katika msimu hu wa sherehe.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi Ijumaa Boinnet aliwataka Wakenya kuendelea na shughuli zao za sherehe bila wasiwasi wowote.

Alitoa wito kwa waendeshaji magari kuwa waangalifu barabarani ili kuzuia ajali ambazo hutokea katika msimu kama huu.

“Tumejipanga kuhakikisha kuwa kila mmoja wetu yu salama. Hata hivyo, nawataka wenye magari kuzingatia sheria za trafiki ili kuzuia ajali ambazo zinaweza kuleta maafa,” akasema.

Bw Boinnet pia aliwataka watembeaji kwa miguu kuwa waangalifu, akisema wao huchangia asilimia 40 ya vifo kutokana na ajali humu nchini.

Alisema taifa hili limepiga hatua kubwa katika vita vya kupambana na ugaidi, akiongeza kuwa visa vya mashambulio ya kigaidi vimepungua katika miaka ya hivi karibuni.

“Maeneo ambako mashambulio ya kigaidi yalikithiri sasa yanafurahia utulivu. Hii ni kwa sababu tumewatuma maafisa wetu katika maeneo hayo kulinda doria,” akasema huku akiandamana na Mkurugenzi Mkuu wa Halmshauri ya Usalama Barabarani (NTSA) Francis Meja.

Bw Meja alisema idadi ya watu wanaofariki kutokana ajali za barabarani zimepungua kwa kiwango kikubwa ndani ya kipindi cha miaka minne iliyopita.

Alisema visa hivyo vilipungua kwa kima cha asilimia 19.7 mwaka huu.

“Kupungua kwa visa hivi kunamaanisha kuwa kampeni ya kuhimiza usalama barabarani imezaa matunda. Hata hivyo, juhudi hizo zinapasa kuendelezwa zaidi kwa ushirikiano na wadau wote,” Bw Meja akaeleza.

Aliwaonya wenye magari ya uchukuzi dhidi ya kuongeza nauli kiholela akisema wale watakaopatikana wakifanya hivyo wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

Bw Meja alisema NTSA imetoa leseni za uchukuzi (TLB) kuwa magari ambayo yameafikia kanuni ziliwekwa. Magari hayo yanajumuisha yale ambayo yanahudumu katika ruti za mashambani.

“Tumetoa leseni kwa magari ya uchukuzi wa umma kwa misingi ya jinsi yalivyozingatia kanuni zilizowekwa. Hataruhusu gari lolote kusafirisha watu kutoka mijini kwenda mashambani,” akasema.

Bw Meja, vile vile, alitoa wito kwa wahudumu wa bodaboda kuzingatia sheria za barabarani na kuvalia kofia ya kinga na jaketi za kiakisi mwangaza.