• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
Krismasi ya jua kali

Krismasi ya jua kali

Na COLLINS OMULO

MVUA inatarajiwa kupungua katika maeneo mengi wiki hii wakati Wakenya wanapoendelea kujiunga na jamaa na marafiki kwa sherehe za Krismasi, Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa imesema.

Kaimu Mkurugenzi wa idara hiyo, Bi Stella Aura, alisema mvua itapungua katika maeneo mengi nchini wiki hii baada ya maeneo kama vile Rift Valley na ukanda wa Pwani kushuhudia mvua kubwa wiki iliyopita.

Kulingana na utabiri wa hali ya hewa ya siku tano kuanzia Desemba 22 hadi 26, kaunti za Turkana, Pokot Magharii na Samburu zitashuhudia jua mchana na mawingu usiku katika kipindi hicho.

Kaunti za Nairobi, Nyandarua, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, na Tharaka Nithi zitakuwa na mawingu asubuhi kisha jua kuwaka siku nzima. Katika nyanda za chini za kusini mashariki mwa Kenya ambapo kuna kaunti za Kajiado, Kitui, Makueni, Machakos na Taita Taveta kutakuwa na jua kuanzia asubuhi.

Hali sawa na hii itashuhudiwa katika kaunti za Siaya, Kisumu, Homa Bay na Migori zinazopakana na Ziwa Victoria.

Kaunti za nyanda za juu za Rift Valley pia zitashuhudia jua asubuhi na mchana. Kaunti hizo ni Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo-Marakwet, Nandi, Laikipia, Nakuru, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma na Busia.

Katika eneo la kaskazini mashariki, Kaunti za Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa na Isiolo zitashuhudia jua asubuhi na mawingu usiku katika kipindi hicho chote. Ukanda wa Pwani unaojumuisha kaunti za Mombasa, Tana River, Kilifi, Lamu na Kwale utakuwa na jua asubuhi katika sehemu mbalimbali, na manyunyu ya mvua Jumatano asubuhi.

Idara hiyo hata hivyo ilisema huenda mvua kubwa ikaanza kunyesha tena mwanzoni mwa mwaka ujao haswa katika maeneo ya Bonde la Ufa, Kaskazini na Kati

Maeneo ambayo huenda yakashuhudia mvua baadaye ni Bomet, Elgeyo Marakwet, Trans Nzoia, Uasin Gishu, Nakuru, laikipia, Nyandarua, Kirinyaga, Meru, Tharaka Nithi, Embu, Kiambu, Nairobi, Murang’a na Nyeri.

You can share this post!

Maraga atoka hospitali, mkewe bado atibiwa

Mahangaiko ya Krismasi

adminleo