• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:55 AM
Mahangaiko ya Krismasi

Mahangaiko ya Krismasi

Na MOHAMED AHMED

KAMPUNI za mabasi jijini Mombasa zinafurahia kunoga kwa biashara zao kufuatia idadi kubwa ya wasafiri wanaoelekea bara kwa ajili ya sherehe za Krismasi. Pitapita ya Taifa Leo katika vituo vya mabasi jijini humo iliona abiria waliokuwa wamejaa pomoni kwenye vituo hivyo huku wengi wakipigania nafasi kwenye mabasi hayo.

Katika kampuni ya mabasi ya Mash East Africa usimamizi wa kampuni hiyo ilisema kuwa mabasi yao yamejaa hadi Januari 10 mwaka ujao.

Akizungumza katika mahojiano nje ya afisi zao, mkurugenzi wa kampuni hiyo ya usafiri Said Abeid alisema kuwa idadi kubwa ya wasafiri hao ni wale wanaoelekea maeneo ya Nairobi, Kisumu, Kakamega na Mumius miongoni mwa maeneo mengine.

“Tanashukuru Mungu kwa kutufungulia milango ya biashara wakati wa msimu huu licha ya kuwa na changamoto ya ushindani kutoka kwa usafiri wa reli ya SGR. Kufikia sasa tumekuwa na idadi nzuri ya abiria,” akasema Bw Abeid.

Alisema kuwa kwa sababu ya msimu huu wa sherehe wamelazimika kupandisha tikiti kwa Sh200 hadi Sh400.

Kwa sasa, kwa mfano kusafiri kutoka Mombasa hadi Nairobi inagharimu Sh1400 ambapo kwa siku za kawaida ilikuwa ni Sh1, 200.

Aidha, kutoka Mombasa hadi Kisumu wasafiri wanaosafiri na mabasi ya kampuni hiyo wanalipa Sh2, 200 ambapo kwa kawaida hulipa Sh2, 000.

“Kwa sababu ya hali ngumu ya maisha imetulazimu sisi pia tupandishe bei ya usafiri ili tuweze kujikimu na hilo limefanyika kwa sababu ni msimu wa siku kuu,” akasema.

Katika kampuni ya Coast Bus, usimamizi wa kampuni hiyo ulisema kuwa wamelazimika kuongeza idadi ya mabasi ili kuhakikisha kuwa abiria wanapata nafasi za kutosha kufikia maeneo yao wanayoelekea.

Afisa msimamizi wa kituo hicho Hali Sadia alisema kuwa licha ya kuongeza mabasi, idadi ya abiria bado ni kubwa.

“Idadi kubwa ya abiria ndio changamoto pekee tunayopambana nayo ndiposa tunajaribu kupeleka mabasi kule ambapo tunaona yanahitajika zaidi,” akasema.

Hata hivyo abiria walioongea na Taifa Leo walilalamikia kuongezwa kwa bei ya usafiri huku wengine wakisononeshwa na idadi ndogo ya magari.

“Magari ni kidogo na hali hii imepelekea wengine wetu kukwama. Natafuta njia mbadala ya kufika kule ninapoenda. Lakini hali imekuwa ngumu haswa kwa sisi ambao hatukupata nafasi za mapema za mabasi,” akasema Eunice Chanya mmoja wa abiria.

You can share this post!

Krismasi ya jua kali

Walimu wa shule miamba wa zamani wahepa wanahabari

adminleo