LAMU: Waapa kupiga vita mradi mkubwa wa nishati ya makaa
Na KALUME KAZUNGU
WATETEZI wa mazingira, viongozi wa kidini na baraza la wazee katika Kaunti ya Lamu wameahidi kuendelea na shinikizo za kupinga mradi wa nishati ya makaa ya mawe 2019.
Wakizungumza wakati wa kongamano la kufunga mwaka lililoandaliwa katika hoteli ya Mwana Arafa mjini Lamu jana, wanaharakati, viongozi wa kidini na wazee hao walisema kamwe hawatalegeza kamba katika kampeni yao ya kupinga mradi wa nishati ya makaa ya mawe walioutaja kuwa sumu kwa mazingira na afya ya wenyeji.
Mradi huo wa Sh200 bilioni unanuiwa kujengwa katika eneo la Kwasasi, tarafa ya Hindi, Kaunti ya Lamu.
Mradi huo uko chini ya ufadhili mkuu wa kampuni ya Amu Power na kufikia sasa tayari ekari 975 za ardhi zimetengwa kijijini Kwasasi ili kufaulisha ujenzi wa mradi huo.
Mwenyekiti wa Muungano wa Save Lamu, Bw Mohamed Abubakar, alisema kamwe hawatatishwa na dhuluma ambazo zimekuwa zikitekelezwa na walinda usalama dhidi ya wanaharakati wanaopinga miradi yenye athari kwa mazingira Lamu.
Bw Abubakar alisema kupitia ushirikiano na viongozi wa kidini na baraza la wazee wa Lamu, wataandaa kampeni kali ifikapo 2019 itakayohakikisha mradi wa nishati ya makaa ya mawe hauendelezwi Lamu.
“Leo tumekuja pamoja kama wanaharakati, viongozi wa kidini na wazee wa Lamu. Tumeafikiana kwamba tutaungana na kuendeleza kampeni kabambe za kupinga mradi wa nishati ya makaa ya mawe ifikapo 2019. Hatatutalegeza kamba wala kuogopa vitisho kutoka kwa walinda usalama,” akasema Bw Abubakar.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee, Kaunti ya Lamu Sharif Salim alisema ni vyema serikali kuheshimu hisia za wakazi wa Lamu.
Bw Salim alisema haelewi nia ya serikali kujaribu kulazimishia wakazi wa Lamu mradi wenye athari mbaya.
Alisema ni vyema malalamishi ya wakazi yazingatiwe na mradi mbadala na salama wa kuzalisha kawi upelekwe Lamu badala ya nishati ya makaa ya mawe.
“Serikali iheshimu hisia za wakazi wa Lamu. Si vyema makosa yaliyotekelezwa serikali ilipoanzisha mradi wa bandari ya Lamu (LAPSSET) yarejelewe kwa miradi mingine inayonuiwa eneo hili. Hadi sasa waathiriwa wa LAPSSET bado wanalalamika. Serikali isilazimishie wakazi miradi. Cha msingi ni hisia za wakazi zizingatiwe na matatizo yatatuliwe,” akasema Bw Salim.
Naye Ustadh Said Khitamy alisema iwapo mradi wa nishati ya makaa ya mawe utajengwa Lamu utaathiri sekta muhimu ambazo ni uti wa mgongo wa Lamu, hasa uvuvi.
Alisema endapo mradi huo utafaulu kujengwa Lamu, samaki wa baharini na viumbe wengine huenda wakafariki kutokana na sumu kutoka kwa kiwanda hicho.
Bw Khitamy alisisitiza haja ya wakazi wa Lamu kuongea kwa sauti moja ili kilio chao kisikike ulimwenguni kote.
“Kwa nini tusukumiwe mradi wa nishati ya makaa ya mawe? Hii ni njama ya vizazi vya Lamu kumalizwa na hatutakubali,” akasema Bw Khitamy.