Habari Mseto

Purukushani harusini kidosho akidai kuwa mke wa bwana harusi

December 31st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na MAGDALENE WANJA

Kizaazaa kilitokea harusini mjini Nakuru wakati mwanamke mwenye umri wa miaka 21 alijitokeza akidai kwamba alikuwa mke halisi wa bwana harusi.

Harusi kati ya Bw Dennis Kinyanjui na Bi Agnes Wangari ilikuwa ikiendelea katika kanisa la ACK Nakuru eneo la Pipeline wakati mwanamke huyo alifika akiandamana na mamake na marafiki zake.

Bi Agnes Wanjiru alidai kuwa alikuwa kwenye ndoa na Bw Kinyanjui kwa muda miaka mitatu na kuwa alikuwa na mimba ya miezi sita.

Wakazi walivutiwa na kivangaito hicho mtaani Pipeline, Nakuru. Picha/ Magdalene Wanja

“Nina stakabadhi nyingi za kuonyesha kwamba ni mume wangu zikiwemo zile za bima ya NHIF ambazo alitia sahihi ,” alisema Bi Wanjiru.

Bi Wanjiru alishangaa kwa nini harusi hiyo ilikuwa ikifanyika katika kanisa la ACK Jehovah Shammah ambalo ni tofauti na lile la Saints Payers Fellowship lililoko katika eneo la Ponda Mali ambako alikuwa afunge pingu za maisha na mwanamume huyo.

Kulinganma na mamake Wanjiru, Bi Lucy Wanjiku, Bw Kinyanjui pamoja na familia yake walikuwa wamemtembelea hapo hawali wakimuomba kuwapa ruhusa kufanya harusi na wakakubaliana.

Kanisani ambapo harusi hiyo ilifanyika. Picha/ Magdalene Wanja

“Tulishangaa tu tulipoarifiwa kwamba Bw Kinyanjui anamuoa mwanamke mwingine,” alisema BiWanjiku.

Kizaazaa kiliibuka wakati vikundi kutoka pande zote vilikabiliana katika kuingilia huku kikundi kimoja kikizuia kingine.

Bi Wanjiru alitaka kuingia kanisani na kusimamisha harusi hiyo.

Gari lililobandikwa ujumbe wa harusi ya Agnes na Dennis. Picha/ Magdalene Wanja

Wakati majibizano hayo yalipokuwa yakiendelea, harusi ilifanyika katika kanisa hilo chini ya ulinzi mkali wa wafuasi wao.

Bi Wanjiru alilazimika kukwea kiingilio cha kanisa hilo ila harusi ilikuwa tayari imefanyika.

Maharusi hao waliondolewa kanisani chini ya ulinzi huku gari walilotumia likiendeshwa kwa kasi.