Habari za Kitaifa

Ogolla ni mkuu wa kwanza wa KDF kufariki akiwa mamlakani

April 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

Na BENSON MATHEKA

JENERALI Francis Ogolla ni mkuu wa majeshi wa kwanza wa Kenya kufariki dunia akihudumu na wa kwanza kufariki kupitia ajali ya ndege.

Watangulizi wake walistaafu baada ya kukamilisha mihula yao au kwa kufikisha umri wa kustaafu na kuendelea na shughuli za maisha wakiwa raia au kuhudumia taifa katika nyadhifa mbali mbali.

Soma pia Jenerali Ogolla, wanajeshi wengine 9 wafa katika ajali ya helikopta

Jenerali Jackson Kimeu Mulinge aliyeshikilia wadhifa huo kwa miaka mingi zaidi aliteuliwa mwenyekiti wa shirika la serikali kabla ya kujiunga na siasa akiwa mbunge wa Kathiani na kuhudumu kama waziri. Alistaafu siasa na kushughulikia biashara hadi alipifariki Julai 16 2014 akiwa na umri wa miaka 91.

Wakuu wengine wa KDF wastaafu ni Manejerali Mahamud Mohamed, Daudi Tonje, Joseph Kibwana, Jeremiah Kianga, Samson Mwathethe, Julius Karangi, Robert Kibochi.

Jenerali Ogola alikuwa mkuu wa jeshi la Kenya wa 11 tangu 1963. Mkuu wa majeshi wa kwanza mwafrika alikuwa meja jenerali Joseph Ndolo aliyejiuzulu kufuatia tuhuma za kupanga kupindua serikali 1979.

Mtangulizi wake alikuwa Meja Jenerali Robert Bernard Penfold. Kati ya majenerali hao ni watatu wanne waliofariki akiwemo Ogola, Mulinge, Ndolo na Penfold.

Soma pia Helikopta iliyoanguka ilikuwa eneo ambako KDF inakarabati shule kufuatia agizo la Rais