Makala

TAHARIRI: Sheria katu si tatizo, muhimu utekelezaji

January 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA MHARIRI

SHERIA mpya alizoidhinisha rais Uhuru Kenyatta saa chache kabla ya Mwaka Mpya, ni ishara ya kujitolea kwa serikali kuwa na sera muhimu.

Miongoni mwa sheria saba ni ile inayolenga kufanyia marekebisho Shirika la Vijana Kwa Huduma ya Taifa (NYS). Shirika hili limekuwa mojawapo ya yale ambayo yamepoteza mabilioni ya fedha kupitia ufisadi.

Septemba mwaka jana, Benki Kuu ya Kenya ilitangaza kuwa iliadhibu benki tano kwa kukiuka kanuni za kifedha kuhisiana na 3.5 bilioni za NYS.

Washukiwa 52 walikamatwa na kufunguliwa mashtaka mbalimbali kuhusu wizi katika shirika hilo, ambalo lilianzishwa ili kuwapa mafunzo vijana wawe wanaweza kulihudumia taifa, hasa nyakati za dharura.

Lakini inaonekana sheria hiyo haihitajiki katika NYS pekee. Tayari Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi inasema inafuatilia kwa karibu ufujaji wa mabilioni katika idara mbalimbali za serikali kati ya Julai 2017 na Juni 2018.

Ripoti ya kila mwaka ya EACC inaonyesha kuwa taasisi na idara kuu serikalini zimefuja zaidi ya Sh100 bilioni. Kati ya pesa hizo, ni zile zilizokuwa zitumike kununua vitabu kwa shule katika mpango ya Elimu ya Msingi Bila Malipo (FPE).

Kinachojitokeza hapa ni kwamba sheria si tatizo hapa Kenya. Tuko na kila ina ya sheria ambazo zimeundwa na kuidhinishwa na Bunge. Tatizo hasa ni utekelezaji wa sheria hizo. Tuna maafisa wa EACC ambao huchunguza na kuikabidhi idara ya Upelelezi wa Jinai faili kisha zikawasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma. Washukiwa hukamatwa na kupeleka mahakamani. Mwishowe, washukiwa hao hutembea barabarani na kuendelea kupora mali ya umma, huku wakiwaandama waliojitolea kufichua maovu yao.

Kwa hivyo ni vizuri kwamba tunabuni sheria za kukabili maovu kama vile ufisadi. Lakini sheria hizo zitakuwa hazina maana kama zitakuwa tu kwenye nyaraka ilhali hakuna anayezitekeleza ipaswavyo.

Mbali na kuwa na sheria, kila idara inayohusika na utekelezaji wa sheria hizo yapaswa kuweka kanuni na mfumo ambapo anayezivunja hasamehewi.

Wakenya ni watu wanaoogopa adhabu kali. Iwapo mtu atajua kwamba akikamatwa kwa kuiba mali ya umma hatasamehewa na yeyote na kesi yake itakamilika katika kipindi cha wiki mbili au tatu, atafikiri mara mbili kabla ya kutekeleza wizi huo.